Ni uamuzi sahihi kufuta GPA na kurudisha madaraja katika ufaulu

22Jan 2016
Mhariri
Nipashe
Ni uamuzi sahihi kufuta GPA na kurudisha madaraja katika ufaulu

GAZETI hili jana lilimkariri Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, akitangaza kuwa amefuta mfumo wa matokeo ya GPA kwa wanafunzi wa kidato cha nne, sita na ualimu na kurudisha ule wa zamani wa madaraja.

Mbali na hatua hiyo, Ndalichako ameagiza kuondolewa kwa mtihani wa pili (paper two) kwa watahiniwa binafsi ambao ulianza mwaka 2014.
Profesa Ndalichako alisisitiza kuwa amechukua hatua hiyo kutokana na kugundua kuwa kuna baadhi ya watu wanaotaka kuchezea mfumo wa elimu nchini.
Serikali imechukua hatua hiyo, kufuatia baada ya kilio cha muda mrefu kutoka kwa wadau mbalimbali waliokuwa wanapinga hatua ya serikali kuweka madaraja.
Hata hivyo, serikali ya awamu ya nne, ambayo ndiyo ilileta mfumo wa GPA, ilisema ilifanya hivyo kwa lengo la kuongeza ufaulu katika mitihani.
Hali hiyo ilichangiwa zaidi kutokana na miaka ya karibuni wanafunzi wengi kufeli mitihani ya taifa. Hatua hiyo ilisababisha malumbano makubwa kutokana na baadhi ya watu huku baadhi wakiamini ilikuwa inashusha zaidi kiwango cha elimu na kwamba taifa lingejikuta linatengeneza wajinga badala ya kuwa na wanafunzi wanaofaulu kutokana uwezo wao wa darasani.
Serikali ya awamu ya nne, kwa upande wake, nayo ilikuwa na mikakati kamambe ya kupandisha kiwango cha ufaulu ndiyo maana ikaingiza sekta ya elimu kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Akitangaza hatua hiyo, Profesa Ndalichako alisema kuna mgongano mkubwa katika upangaji wa GPA.
Waziri alitolea mfano kuwa kidato cha nne ufaulu unaanzia 3.6-5, kidato cha sita katika daraja hilo ni 3.7 – 5 wakati ufaulu kama huo kwa mafunzo ya walimu unaanzia 4.4 – 5, ambao aliuelezea kuwa ni mkanganyiko mkubwa unaozalisha watu wasio na ubora katika kiwango husika.
Profesa Ndalichako anaeleza kuwa wanafunzi wengi waliopita kwenye mfumo wanakuwa na kiwango kidogo cha uelewa.
Anaamini kuwepo kwa gredi E kwenye alama za ufaulu wakati haihesabiki kwenye upangaji wa GPA, kunawafanya watahiniwa waliopata E kujiona wako bora kuliko wenye D mbili na F zote, ambao pia wanahesabiwa wamefaulu.
Profesa Ndalichako alisema Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) walimweleza kuwa walianzisha utaratibu wa GPA kutokana na maoni ya wadau licha ya kwamba hakupewa ushahidi wa maelezo ya wadau hao.
Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na tatizo kubwa la uendeshaji wa elimu nchini kuingiliwa na wanasiasa. Wanasiasa hawa wamekuwa wakija na mawazo mengi ya kuendesha elimu kwa nia ya kufurahisha wapigakura.
Vitendo hivi vimechangia kushusha kiwango cha elimu na shule za serikali ziko kwenye hali mbaya zaidi.
Katika miaka ya nyuma ilikuwa fahari zaidi kwa mzazi kusomesha mtoto kwenye shule za serikali lakini hali ni tofauti katika siku za karibuni kwani wazazi wengi wanapeleka watoto wao kwenye shule za binafsi.
Shule za serikali ziko katika hali mbaya kwa mfano Ilboru, Kibaha, Mzumbe, Old Moshi, Msalato, Kilakala, Weruweru, Malangali na Milambo ambazo katika miaka ya nyuma zilikuwa zinasifika kwa kutoa elimu bora, hivi sasa zimeporomoka na kupoteza sifa hiyo .
Pia serikali hivi karibuni ilikuja na mpango wa kujenga shule za sekondari za kata, ambao ulifanikiwa kwa shule hizo kujengwa kwenye maeneo mengi nchini.
Bahati mbaya shule hizi zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya ukosefu wa samani na vifaa.
Tunafahamu kuwa serikali imekuja na mpango wa elimu bure lakini tunashauri kuwa mazingira ya shule hizi yaimarishwe ili kutoa elimu bora.
Pamoja na hayo, tunaishauri serikali iweke mkazo wa kupata wanafunzi bora badala ya kutafuta njia za kubeba watu ili kuonyesha kuna ufaulu mkubwa.