Kauli hizi timu zinapofungwa ziepukwe

16Apr 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Kauli hizi timu zinapofungwa ziepukwe

LIGI Kuu Bara inakwenda kwenye hatua za lala salama, huku pia ushindani ukizidi kuongezeka.

Kileleni mwa msimamo, Simba, Yanga na Azam zinafukuzana kuwania taji linaloshikiliwa na Wanajangwani.

Kuna timu ziko salama, kwamba zina uhakika wa kucheza ligi msimu ujao. Lakini, mkiani kuna vita nyingine, siyo ya ubingwa, bali kubaki kucheza ligi msimu ujao.

Ugumu wa ligi wakati ikielekea ukingoni ni kwamba, hadi sasa hakuna timu iliyojihakikishia kutwaa taji. Mkiani nako, hadi sasa hakuna timu ambayo tunaweza kuihukumu kuwa tayari imeshashuka daraja.

Kwenye ushindani wowote ule hasa timu zinapofukuzana kwa karibu kuwania taji au kuepuka kushuka daraja, mambo mengi hujitokeza.

Wiki hii tulishuhudia mechi za viporo za timu za Yanga na Azam FC. Timu hizi zilikuwa zikicheza mechi hizo baada ya ratiba ya mechi zao kupanguliwa ili kuzipa fursa ya kushiriki michuano ya Klabu Afrika.

Mabingwa Yanga walicheza na Mwadui FC ya Shinyanga na Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar.
Sahau mechi ya Azam na Mtibwa iliyomalizika kwa Lambalamba kushinda bao 1-0.

Mechi ya Yanga na Mwadui, haikumalizika bila lawama na maneno kutoka kwa mashabiki na hata baadhi ya viongozi.
Katika mechi hiyo, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui, ushindi ambao upande wa upinzani kupitia kocha Jamhuri Kihwelo ulilalamika.

Kama tulivyosema awali, ushindani ni mkubwa kuelekea mwisho wa msimu, ndivyo inavyoonekana kwenye mechi ambazo matokeo yake yana nafasi kubwa ya kuamua nani atakuwa bingwa.

Ingawa malalamiko kwenye ligi yetu ni sehemu ya utamaduni, lakini yanapoachwa kuendelea kutolewa kila wakati, yanaifanya ligi kupoteza mvuto.

Kauli ya kocha wa Mwadui, Kihwelo kwamba Yanga ilibebwa kwenye mechi hiyo na kupata, siyo ya kimichezo.

Hatumzui kocha huyo kulalamika pale anapoonea timu yake inaonewa, lakini kitendo cha kuzungumza na vyombo vya habari na kukosoa matokeo hayo, badala ya kulalamika mbele ya vyombo husika ni kwenda kinyume na taratibu za mchezo wa soka.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kama msimamizi wa mchezo wa soka, lilipaswa kukemea kauli za makocha na wachezaji wanaoshawishi mashabiki kuamini matokeo hupangwa au waamuzi kupendelea.

Kwa wenzetu wanaoheshimu nadhamu ya mchezo wa soka, kauli kama ya Kiwhelo kuwa Yanga inabebwa, ingekuwa tayari imekemewa na mhusika kutakiwa kutoa maelezo.

Tumeshuhudia wachezaji, makocha na hata viongozi wakitozwa faini kubwa kwa makosa ya kutoa kauli zinazoashiria kulikuwa na hujuma kwenye mechi.

Hata kama kweli mwamuzi alikosea au kupendelea, kuna taratibu husika mlalamikaji anapaswa kwenda kuzipelekea na siyo kuzungumza moja kwa moja na vyombo vya habari na kutoa tuhuma ambazo wasimamizi wa mchezo wa soka TFF hawana.

Ili kuepusha kauli kama hizo na nyingine nyingi zitakazokuja kuelekea mwisho wa msimu, TFF iwe makini kuwakemea makocha na viongozi wanaotoa kauli za ushawishi wa kuamini matokeo nje ya uwanja.

Kuendelea kusikilizwa kwa kauli kama hizo bila hatua kuchukuliwa, tafsiri yake ni kwamba soka letu limejaa ubabaishaji na hata bingwa hupatikana kwa 'mipango'.

Ikumbukwe kuwa, soka letu lina wachezaji wa kulipwa kutoka mataifa mbalimbali, hivyo ili kulinda heshima ya mchezo husika na hata utamaduni wa nchi, ni vizuri makocha wakawa makini na kauli wanazotoa timu zao zinapofungwa.