Ukiona mkeo anatoa siri zako za ndani jichunguze!

03Apr 2016
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Ukiona mkeo anatoa siri zako za ndani jichunguze!

MPENZI Msomaji, mwaka jana niliandika makala safu hii ambapo jamaa alikuwa akilalamikia tabia ya mkewe ya kutoa mambo ya ndani ya nyumba na kuyapeleka nje, mengine yakileta chuki kwa ndugu.

Jamaa huyo katika ujumbe wake mfupi simu ya kiganjani alisema hivi; Mimi naitwa Jumanne Abdalla napatikana Kibaha Maili Moja.

“Mimi nimeoa mke lakini cha ajabu mambo yetu ya ndani huwa anayapeleka kwao mpaka inafikia kipindi mengine yanaleta chuki kwa ndugu zake. Nikimuonya ataomba msamaha, lakini kesho atarudia tena mpaka sasa kumekuwa chuki kubwa na mimi mpaka nakosa amani na ndoa yangu. Naomba ushauri.(0713811217).”

Kabla sijakumbushia machache niliyomshauri katika makala niliyochapisha kwenye safu hii Januari 17, 2016 ikiwa na kichwa cha maneno, “Tabia hii ya mke wangu inanikosesha amani ya ndoa! Hebu msikie msomaji wetu mzuri wa safu hii aliyebahatika kuisoma makala ile anavyomshauri mwenzetu huyo.

Naitwa Mutechura Vermundus; baba huyu ambaye mkewe anaweka mambo ya kifamilia sebuleni (hadharani), afanye yafuatayo ili kutibu hali ya mkewe:

1. Yeye mwenyewe baba ajichunguze kasoro zake kiutawala na kiuchumi zinazopelekea mke kutoa siri zao nje.
2. Huyu baba ampende mkewe kwa pendo la dhati. Upendo hauhitaji fedha, ni jambo la hulka tu.
3. Mipango ya kifamilia aipange mwenyewe asimshirikishe mkewe kwa kipindi cha miezi sita, aongeze utendaji wa kazi. Mke aone tu anaambiwa kutenda bila kushirikishwa ndio atapata funzo la kuacha kuanika yale ya familia.(0766219458).

Huo ndio ushauri wa msomaji wetu aliompa ndugu yetu huyo kuhusiana na sekeseke hilo. Nampongeza sana, utamsaidia. Mimi nilimshauri mengi ila hapa nikumbushie machache kwa wale ambao hawakubahatika kuisoma makala ile. Kwanza nilitoa tafsiri ya tabia kama ilivyotoholewa katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la pili la Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili, Dar es Salaam.

Tabia:Ni mazoea yanayotokana na kurudiarudia hali, mwenendo au matendo.
Kwa tafsiri hii, najaribu kuona ukweli unaojitokeza katika malalamiko ya jamaa hapo juu kwamba tabia ya mkewe ya kutoa habari za ndani ya familia kwa watu wengine imekuwa inajirudiarudia hata pale anapomkanya mara kwa mara.

Baada ya kupata ujumbe wa kijana huyo kupitia simu ya kiganjani, nilimpa ushauri ufuatao; kwamba hiyo ni tabia aliyotoka nayo huko kwao. Ndio maana kabla ya kuoa yafaa uchunguze tabia ya mwenzio.

Ingawa tabia zingine hujificha au ni vigumu kuzirekebisha kutokana na kujikita kwenye uasili, lakini jitahidi pambana na ikiwezekana itisha vikao vya ndugu aonywe, anaweza kubadilika.

Ni ushauri niliompa kwa haraka haraka, lakini bado nilidhani tatizo la bibie huyo lina chimbuko, siyo bure. Kijana huyu akijaribu kuchimbua uasili wa familia ya mkewe, anaweza kugundua kwamba huenda tabia hiyo ya kuvujisha siri za ndani ya nyumba, ameirithi toka kwa mama yake mzazi, au imeanzia kwa bibi mzaa baba au mzaa mama au upande wa baba na kadhalika.

Huo ni mnyororo ambao hauwezi kukatika labda kwa maombi. Na tabia, kibiblia ni roho. Ni kitu kinachotoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine na kuleta madhara. Kwa mfano, kama mama mzazi wa binti alikuwa na tabia hiyo, na binti wakati anakua alikuwa akiona mama yake akifanya vituko kama hivyo, kwanini binti asiviige?

Chanzo cha matatizo wakati mwingine ni wazazi wetu. Kama wazazi hawakuwalea vema watoto, matokeo yake ndio hayo huwa mwendelezo wa madhara hata ukubwani. Jamaa anasema humkanya mkewe anaona kabisa amemwelewa lakini baada ya muda hurudia makosa yale yale.

Hata yeye mwenyewe (binti) anajishangaa kwanini anarudia yale yale aliyokatazwa. Hiyo ni roho inayomfuatilia msichana huyo ambayo inatokana na misingi mibovu aliyokulia.

Hata Mungu ameweka wazi katika moja ya maandiko yake kuhusu misingi kwamba kama haikuwekwa imara, lazima italeta madhara na huwezi kumlaumu mtoto ambaye hukumjenga kitabia.

Anasema; “Misingi ikiharibika, mwenye haki atafanya nini?”. Mtoto anayo haki ya kuishi maisha mazuri yenye tija. Mzazi ndiye mwenye wajibu wa kumjengea misingi mizuri pamoja na serikali kwa maana ya malezi bora. Sasa kama mtoto hakuandaliwa misingi mizuri ya malezi, akiharibika kitabia, nani wa kulaumiwa?

Msomaji wangu, kabla ya kuoa au kuolewa kwenye familia fulani, chunguza kwanza. Mfano, tabia; je, ni familia ya aina gani? Walevi, waabudu matambiko, washirikina, wambeya, wahuni, washerati, wafitini, wana wivu, wapole, wacha Mungu na kadhalika.

Je, una jambo la kimaisha linakutatiza? Lete tujadiliane. Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com au flora.wingia@guardian.co.tz