Watumishi hewa wanalelewa na nani?

03Apr 2016
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Watumishi hewa wanalelewa na nani?

JUNI mwaka 2012, aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk. William Mgimwa, alisema serikali ilikuwa imepoteza zaidi ya Sh. bilioni 5.4 kwa kulipa mishahara kwa watumishi hewa 9,949 katika kipindi cha miezi mitano tu.

Marehemu Dk. Mgimwa akasema wizi huo ulikwamisha utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo ambayo ingegharamiwa kwa fedha hizo, ambazo walilipwa wafanyakazi hewa.

Kauli ya Dk. Mgimwa ilikuja ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja kupita tangu aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kutoa agizo la kudhibiti wafanyakazi hewa katika wizara na idara za serikali.

Nakumbuka Machi 2011, Rais Kikwete aliamuru kufanyika kwa ukaguzi katika idara zote za serikali kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba kiasi cha Sh. bilioni 9 kilikuwa kimelipwa kama mishahara kwa wafanyakazi hewa katika wizara tatu tu za Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Katiba na Sheria na Afya na Ustawi wa Jamii.

Rais akasema wahusika wa wizi huo walipaswa kubainishwa, ikiwa ni hatua ya kukomesha mara moja wizi wa fedha za umma kupitia mishahara hewa na kwamba serikali haipaswi kuwaruhusu watu ambao wanaiibia kuendelea kufanya kazi za umma.

Cha ajabu ni kwamba pamoja na jitihada za serikali ya awamu ya nne za kudhibiti wafanyakazi hewa, tatizo hilo limeendelea kuwa kubwa zaidi na sasa imebainika kwamba utafunaji wa fedha za umma umeongezeka zaidi.

Hayo yamebainishwa kwenye baadhi ya mikoa kufuatia agizo la Rais John Magufuli kuwapatia siku 15 wakuu wa mikoa wote kuhakikisha wanabaini wafanyakazi hewa waliopo kwenye idara na taasisi za serikali nchini, mara baada ya kuwaapisha katikati ya mwezi uliopita.

Na kufikia katikati ya wiki, zaidi ya watumishi hewa 1,850 walikuwa wamebainika katika idara na taasisi za serikali kwenye mikoa mbalimbali nchini ambao wameisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 3.6.

Taarifa iliyowasilishwa kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, watumishi hewa waliobainika hadi sasa ni 1,850 ambao taarifa za awali zinaonyesha kuwa kwa nyakati tofauti wamelipwa Sh. 3,562,670,000.

Wizi huo umegundulika Simiyu (33) ambao walilipwa Sh. milioni 320.993, Tabora (48) walilipwa Sh. milioni 118, Tanga (24) na Lindi (57) waliolipwa Sh. milioni 36, Katavi (21) walilipwa Sh. milioni 120 kwa miezi sita, Kagera (14) ambao walilipwa Sh. milioni 49. Geita (wanane) na Manyara watano.

Mingine ni Arusha watumishi hewa 270 walibainika katika kipindi cha wiki mbili waliosababisha upotevu wa Sh. bilioni 1.188 kwa mwezi Machi, Singida watumishi hewa 202, Kigoma watumishi hewa 171 waliosababisha hasara ya Sh. milioni 114.6 kwa mwezi.

Mikoa mingine ni Kilimanjaro wenye watumishi hewa 111 ambao walilipwa Sh. milioni 281.4 kwa mwezi mmoja na Dodoma watumishi hewa 101 waliolipwa Sh. milioni 297 kwa muda wa miezi sita.

Nimetaja mikoa michache, lakini kwa ujumla ni kwamba watumishi hewa wametafuna fedha nyingi za umma. Je, ni nani ambaye amewalea hadi sasa licha ya serikali kufanya kila njia na kwa muda mrefu kuhakikisha hawapo kwenye orodha ya watumishi wa umma?

Hivyo juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano ziungwe mkono hasa kwa kuzingatia kwamba kuendelea kukumbatia watumishi hewa ni kukwamisha maendeleo ya nchi hii ambayo watu wake wengi ni maskini.