Mamlaka hiyo kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Irene Isaka, inasema kuwa hatua hiyo imetokana na kuwapo kwa mikataba yenye utata, ambayo mifuko hiyo imeingia na taasisi za umma, wafanyabiashara na watu binafsi, hivyo kusababisha utata pamoja na hasara.
Isaka alisema SSRA ilianza kazi hiyo tangu Januari, mwaka huu, likiwa ni agizo kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na kwamba ukaguzi huo ukibarikiwa na bodi. Hatua ya mamkala hiyo kuikagua mikataba ya mifumo ya hifadhi ya jamii ni nzuri na lengo lake ni la msingi.
Mamlaka hiyo inasimamia mifuko mingi ikiwamo NSSF, PPF, LAPF, PSPF na GEPF, hivyo itakuwa na taarifa za kina kuhusiana na jinsi baadhi ya mikataba inavyoathiri mifuko hiyo.
Baadhi ya mifuko hiyo inatekeleza miradi mikubwa ambayo imekuwa ikilalamikiwa na watu kadhaa wakiwamo wanachama wake kuwa mikataba hiyo ina utata na mingine ina harufu ya ufisadi. Hatua ya SSRA ya kuchunguza mikataba hiyo imekuja wakati mwafaka na ukweli wake utabainika kisha hatua kufuata.
Sio nia yetu kueleza kila mfuko unatekeleza miradi gani ambayo inadaiwa kuwa na utata au harufu ya ufisadi, isipokuwa kutahadharisha kwamba mifuko ya hifadhi ya jamii inatakiwa kuwa makini katika kusaini mkitaba na taasisi na watu binafsi.
Itakumbukwa kwamba lengo la msingi la kuanzishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ni kuwahudumia wanachama wake na mambo mengine yanakuja baadaye, hivyo, kama kuna miradi inatekelezwa, ni lazima faida inayopatikana iwanufaishe wanachama.
Pale inapotokea kwamba mfuko wa hifadhi ya jamii ukawa katika hali mbaya kifedha na kushindwa kuwahudumia wanachama wake hususan kuwalipa mafao yao wakati unatekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi, basi kuna tatizo ambalo linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Ipo mifuko ambayo imeingia mikataba yenye mibaya na kuisababishia hasara ambayo siyo tu kuwa inaiathiri mifuko yenyewe, bali pia wanachama wake. Kama SSRA imeligundua tatizo hilo, basi zitafutwe njia za kujiepusha na hali hiyo.
Uchunguzi huo kama utabainisha kuwa kuna matatizo makubwa katika mifuko hiyo yanayotokana na mikataba tata na ya kifisadi, itungwe sheria ya kuiongezea meno SSRA katika kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwamo kushauri na kupitia mikataba hiyo kabla ya kusainiwa.
Kushirikishwa kwa SSRA wakati wa kusaini mikataba hiyo kutaisaidia mifuko ya hifadhi ya jamii kupata ushauri mzuri ambao utaipunguzia uwezekano wa kuingia katika mikataba isiyofaa na inayoweza kuisababishia hasara pamoja na athari nyingine.
Tunapongeza hatua hiyo ya SSRA ya kuchunguza mikataba ya mifuko hifadhi ya jamii na kunasema kuwa ina mantiki kwa kuwa itaisaidia mifuko kuepukana na matatizo yasiyo ya lazima ambayo yanaweza kuidhoofisha au kuiua kabisa.
Sisi tungependa kuona mifumo ya hifadhi ya jamii ikiwa imara na kutekeleza miradi inayoiingizia kipato stahiki na hata pale waajiri wanapochelewesha michango ya wanachama, haiathiriki kimapato.










