CUF: Hakuna Rais wala mawaziri Z'bar

08Jan 2016
Nipashe
CUF: Hakuna Rais wala mawaziri Z'bar

Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, kimesema hakuna sababu ya kufungua kesi dhidi ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, juu ya kubakia kwake madarakani wakati kwa mujibu wa Katiba, muda wake umemaliza tangu Novemba 2, mwaka jana.

Katibu Mkuu wa CUF. Maalim Seif Shariff Hammad

“Hatua ya kufungua kesi kupiga serikali ya awamu ya saba kuendelea kubakia madarakani sawa na kupoteza muda kutokana mfumo wa sheria Zanzibar kuathiriwa na mgogoro wenyewe ambao umetokana na kuvunjwa kwa Katiba na sheria,” amesema Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alipokuwa akizungumzia kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kuwa bado ni Rais halali kwa mujibu wa Katiba na wasioamini wana haki ya kwenda mahakamani kwa kuwa ndiyo chombo chenye haki ya kutafsiri Katiba ya Nchi.

Alisema mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, umetokana na kuvunjwa kwa Katiba ya Zanzibar na hakuna chombo chochote cha sheria chenye ubavu wa kumuondoa madarakani Rais hata kama watafungua kesi dhidi ya serikali.
“Tume ya Uchaguzi Zanzibar, imevunja Katiba na sheria na mfumo wa kisiasa umevunja mifumo yote ya kisheria ya kusimamia haki kutokana na uzito wa jambo lenyewe,” alisema Shehe.

Alisema kutokana na mgogoro huo kuwa wa kisiasa, ni muhimu ukamalizwa kisiasa kwa kufuata Katiba na sheria.

Shehe alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kifungu cha 28(2) cha Katiba ya Zanzibar muda wa Rais kubakia madarakani ni miaka mitano na Rais pamoja na Mawaziri wake walifikisha ukomo wa kubakia katika madaraka Novemba 2, mwaka huu.

“Kwenda mahakamani sawa na kuzunguka mbuyu, serikali imefikisha kikomo pamoja na mawaziri wake.

Huwezi kuteuliwa kuwa waziri kabla ya kuwa mwakilishi wakati Baraza la Wawakilishi limevunjwa tangu Agosti 13, mwaka jana,” alisema Shehe.

Alisema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salim Jecha, amevunja Katiba ya Zanzibar na kusababisha nchi kuingia katika matatizo makubwa kwa sababu hakuna kifungu cha Katiba au sheria inayompa uwezo wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu.

“Haiwezekani uwe na serikali bila ya kuwapo Baraza la Kutunga Sheria baada ya Baraza la Wawakilishi kuvunjwa kutokana na kumaliza muda wake,” alisema.
Aidha, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 90(1) cha Katiba ya Zanzibar, Baraza la Wawakilishi lilitakiwa kuundwa ndani ya siku 90 na mwisho wake ulikuwa Novemba 12, mwaka jana.

Shehe alisisitiza kuwa kifungu cha 43 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kimeweka shariti mawaziri watateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Hata hivyo, alisema CUF inaendelea kusubiri maazimio ya mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo wa Uchaguzi Mkuu, lakini alisema muhimu mazungumzo kujali muda na kumalika kwa wakati.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu uhalali wa Serikali yake Kikatiba tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu, Rais Dk. Shein alisema kwa mujibu wa Katiba, bado ni Rais halali pamoja na mawaziri wake.

Dk. Shein alisisitiza kuwa anaongoza nchi kwa mujibu wa Katiba na sheria na kwamba kama si uwezo huo aliopewa Kikatiba, hana sababu ya kukaa madarakani pamoja na serikali anayoiongoza.