Wiki iliyopita tuliona hatua za kuchukua kwa mfanyabiashara wa ngazi yoyote, awe wa kawaida au mwenye mtaji mdogo, wa kati na mfanyabiashara mkubwa, ili bei anayoitoa kwenye zabuni yake ya kununua dhamana za serikali za muda mfupi (Treasury Bills), iweze kushinda.
Tukasema kuwa, katika zabuni yake ya ununuzi wa hati fungani za muda mfupi, anapaswa atoe bei ya chini ili iwe rahisi kuchukuliwa miongoni wa zabuni nyingi zitakazokuwa zimewasilishwa.
Tukasisitiza kuwa, mojawapo ya faida anazotarajiwa kuzipata mfanyabiashara anayenunua dhamana za serikali za muda mfupi ni uhakika wa kulipwa fedha zake na faida yake katika kipindi cha siku ambazo dhamana zitaiva.
Ni vizuri nikaendelea kukumbusha hapa kuwa, dhamana za serikali za muda mfupi ambazo ndizo tunaendelea kuzizungumzia hapa, zinachukua kuanzia siku 35, 91, 182 na 364.
Tukiendelea kuanzia hapa kwa leo tunasema kwamba, mnada wa dhamana za serikali hufanyika kila Jumatano ya kila wiki.
Hivyo ni muhimu kwa mfanyabiashara ama mtu mwingine anayependa kuwekeza kwenye mnada wa dhamana za serikali, akalifahamu hilo.
Aidha matokeo ya mnada hutolewa siku hiyo hiyo ya mnada, kupitia tovuti ya Benki Kuu (BoT) na ofisi zote za mawakala.
Tulisema huko nyuma katika safu hii kwamba, kwa kila mkoa kuna mawakala maalumu walioidhinishwa na BoT (Central Depository Participants ama CPD kwa kifupi).
Hawa wameidhinishwa kushiriki kwenye minada hii moja kwa moja kwa niaba yao wenyewe, pia kwa niaba ya wateja wengine.
Sasa ni katika ofisi za mawakala hawa ambako pia matokeo ya mnada hupatikana.
Na kwa kawaida, malipo ya dhamana za serikali za muda mfupi hufanyika sikumbili baada ya mnada, yaani siku ya Ijumaa kwa hati fungani zilizoiva.
Ndivyo hali ilivyo kwa mfanyabiashara anayewekeza kwenye ununuzi wa dhamana za serikali za muda mfupi.
Kwa upande wa dhamana za serikali za muda mrefu yaani Treasury Bonds, mfanyabiashara anapaswa kuelewa kuwa, hizo huiva kuanzia kipindi cha miaka miwili, mitano, saba, 10 na miaka 15.
Hivyo, ni muhimu kwa mfanyabiashara anayetaka kuwekeza fedha zake kwenye hati fungani hizi, akavielewa vipindi hivi na kuchagua muda anaoona unamfaa.
Tofauti na ilivyo kwenye dhamana za serikali za muda mfupi, ambazo huuzwa kwa kila punguzo kwa kila Shilingi 100, dhamana za serikali za muda mrefu huuzwa kwa namna tatu.
Pia, hati fungani hizo huuzwa kwa kila punguzo la shilingi 100, kama ilivyo kwenye dhamana za serikali za muda mfupi ama zaidi ya Shilingi 100 na ama sawa na Shilingi 100.
Hii ina maana kuwa, mfanyabiashara anaweza akatoa bei ya punguzo ya Shilingi 100 ama akatoa bei ya Shilingi 100 au zaidi ya Shilingi 100.
Uwekezaji wa dhamana hizo za serikali za muda mrefu, huambatana na riba inayotolewa na BoT, na riba hiyo hutegemea na kipindi ambacho mwekezaji amekichagua.
Tuendelee Ijumaa ijayo.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








