Huduma katika kipindi cha mpito zimepangwa kuanza Jumapili wiki hii. Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Gilliard Ngewe, alitoa rai hiyo juzi baada ya nauli zilizopendekezwa na Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT) kukataliwa.
Mapendekezo hayo yalikataliwa katika mkutano wa wadau wa usafiri, uliofanyika katika ukumbi wa Karimjee. UDA-RT itatoa huduma za kipindi cha mpito.
Alisema katika kuamua suala la nauli, SUMATRA haiwezi kuangalia tu mapendekezo ya waendeshaji, bali inazingatia pia maoni ya wadau, wananchi na hali halisi ya nchi. Aliahidi kwamba maoni na mapendekezo yote yatapewa uzito wakati wa kuamua nauli zitakazotumika. “Sisi ni wadhibiti, maoni yenu yatafanyiwa kazi na endeleeni kujenga utamaduni wa kushiriki majadiliano kama ilivyo hivi leo (juzi). Hii itasaidia mamlaka kufanya kazi zake kwa urahisi na kwa maslahi ya nchi”, alisisitiza.
Amewahakikishia wananchi kuwa nauli zitakazopangwa ndizo tu zitakazotozwa na wenye mabasi na si vinginevyo.
Ngewe pia aliwataka wenye mabasi ya abiria kufuata sheria kwa kutoza nauli elekezi nchi nzima ili kujenga utamaduni wa kufanya biashara yenye maslahi kwa pande zote mbili. Mkurugenzi Mtendaji wa UDA-RT, David Mgwassa, alisifu mchango wa wadau na kuahidi kuutumia katika kupendekeza nauli zenye maslahi kwa pande zote mbili. “Tunathamini maoni ya wadau na tunaomba pia mamlaka izingatie hali ya uendeshaji wa mabasi ili watumiaji na kampuni tuweze kufaidika na mradi mzima,” alisema.
Awali kampuni yake ilipendekeza nauli ya Sh. 1,200 kutoka Kimara hadi Kivukoni na Sh. 700 kutoka Mbezi hadi Kimara. Pia ilipendekeza Sh. 700 na 1,400/- kwa njia za mrisho wa njia kuu. Mapendekezo yote yalikataliwa na wadau katika mkutano huo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Watumiaji Huduma za SUMATRA (SUMMATRA- CCC), Dk. Oscar Kikoyo, aliitaka mamlaka hiyo kuzingatia maoni ya wadau na nauli zinazotumika sasa ndizo zitumiwe na mradi wa BRT ili kuwapunguzia wananchi mzigo.
Amesema nauli zitozwe kwa kilometa au ukanda na kupinga wazo la nauli ya aina moja kwa barabara nzima. “Tunatambua kuwa huu ni uwekezaji mkubwa na kwa maoni umekuja kuboresha maisha ya wananchi. Kwa hiyo nauli za mabasi haya zibaki kama zilizopo,” alisema










