Serikali yajipanga kuwabeba wajasiriamali

13Mar 2016
Efracia Massawe
Nipashe Jumapili
Serikali yajipanga kuwabeba wajasiriamali

SERIKALI imesema inajukumu la kuwaunga mkono wajasiriamali wa ndani kwa kuwaboreshea mazingira ya shughuli zao, hasa walio na nia ya kujaribu ili bidhaa zao zitambulike ndani na nje kwa maslahi ya ndani.

DK. KINGWANGALA

Aidha, imesema itawasaidia wajasiriamali wenye uweze wa kuwekeza ndani ili uchumi wa nchi ukuwe kupitia bidhaa wanazozalisha ambazo zitatambulika kwa kulipa kodi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi jijini, Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk. Hamisi Kingwangala, alisema jukumu la serikali ni kuwekeza kwa wajasiriamali wa ndani ili bidhaa zao kupitia soko la ndani zitambulike badala ya jamii kuendelea kutumia za nje.

“Kama wajasiriamali wanazalisha bidhaa zenye ubora na kuvutia ni lazima soko la ndani litakuwa , vinginevyo tutakuwa tunatwanga maji katika kinu, hivyo wabuni bidhaa nzuri badala ya watumiaji kunufaika na suparmarket za wageni, wajenge mazoea ya kukuza uchumi wa ndani,” alisema Kingwangala.

Naye Muhad Abdillah Gulled aliwashauri wajasiriamali wengine kuzalisha na kubuni bidhaa zinazokidhi viwango vya Mamlaka ya Chakula Tanzania (TFDA), pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili watumiaji wasipatwe na madhara.

Kwa mujibu wa Abdillah, ametoa ajira kwa wafanyakazi 48, lakini ametoa fursa kwa wengie 300, ambao watakuwa kama vibarua katika duka lake.