alilazimika kutengua uamuzi wake wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Taifa
Aidha, katika hali ambayo inaonyesha baadhi ya mawaziri hawajasoma 'msahafu' wa Rais John Magufuli wa kuchukua tu hatua za kinidhamu za kimamlaka kwa watumishi wa umma walioboronga, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe juzi aliagiza kuhamishwa kwa watumishi 15 wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha, na ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma.
Prof. Maghembe amesema watumishi hao 15 wa idara ya Uhasibu wanahamishiwa wizarani wakati uchunguzi dhidi yao ukiendelea!
Na uchunguzi wenyewe ni juu ya tuhuma zipi?
Kuchoma moto kumbukumbu za vikao vya bodi ya wakurugenzi kwa lengo la kuharibu ushahidi wa makosa mbalimbali yakiwemo ya ubadhirifu, miongoni mwa nyingi.
Maamuzi yaliyojaa mapungufu haya ya Waziri Mhagama na Waziri Maghembe, tunaona Nipashe, hayaendani kabisa na kasi ya Rais wa tano Magufuli kutokana na kukosa umakini.
Sababu za kuteunguliwa kwa uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF saa tano tangu akabidhiwe ofisi hazijawekwa wazi japo zinaeleweka, kutegemeana na ufahamu wa mtu katika masuala ya mipaka ya kimamlaka na taratibu za uteuzi wa nafasi nyeti katika utumishi wa umma.
Aidha, uamuzi wa Maghembe ulikuja katika siku ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwakumbusha watumishi wa umma kote nchini kwamba yeyote atakayeharibu kazi atafukuzwa hapohapo alipo na hakutakuwa na uhamisho kama ilivyokuwa imezoeleka katika awamu nne za kwanza za serikali.
Tunakumbuka Nipashe kwamba wakati akiwa katika kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, mgombea wa CCM wakati huo, Rais Magufuli alisema akichaguliwa kuishi katika Ikulu ya Magogoni kwa miaka mitano ya 2015-2020, hakutakuwa na uhamisho wa watumishi walioboronga kama ilivyokuwa imezoeleka.
Ndiyo maana basi tunajiuliza, Nipashe, waziri kama Maghembe anawezaje kuhamisha watumishi aliodai wana tuhuma nzito kama za kuhujumu shirika la umma na si kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi ama kuwafukuza papo hapo?
Hapakuwa na semina elekezi zilizokuwa zikigharimu wastani wa Sh. bilioni 2 kama katika serikali ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, mwaka jana Nipashe tunafahamu.
Semina elekezi, Nipashe tunafahamu pia, ziliondolewa na Rais Magufuli kwa nia njema ya kuondoa matumizi mabaya ya fedha za umma katika nchi ambayo wananchi wake wanakosa huduma nyingi muhimu za kijamii katika nyanja za elimu na afya.
Lakini waliyofanya Mhagama na Maghembe wiki hii yanatufanya Nipashe tujiulize pia kama mawaziri wetu hawaendi vizuri bila semina elekezi; hasa ikizingatiwa kuwa wote wawili walikuwa katika Baraza la Mawaziri la mwisho la Kikwete.










