Kwa mujibu wa TFF, mechi za robo-fainali ya michuano hiyo zitaanza kuchezwa wikiendi ya mwisho ya mwezi huu, Geita Gold FC watachuana na wachimba madini wenzao, Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza Machi 26.
Yanga watakuwa wenyeji wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa wakati Azam FC wakiwakaribisha Tanzania Prisons katika viunga vya Chamazi Machi 31, huku Simba wakicheza dhidi ya Coastal Union jijini Dar es Salaam Aprili 6.
Tukiwa wadau namba moja wa michezo nchini, Nipashe hatuungi mkono namna TFF inavyochezesha droo ya michuano hii ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.
Tunakumbusha kuwa raundi ya kwanza na ya pili ya Kombe la FA msimu huu, ilishirikisha timu za Ligi Daraja la Pili (SDL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Timu za Ligi Kuu zilianzia raundi ya tatu, lakini TFF haijawahi kuweka wazi kwa umma sababu za upangaji wa ratiba ya aina hiyo.
Haijaelezwa, kwa mfano, ilikuwaje wakapanga mechi za mahasimu katika mikoa ya Shinyanga (Stand United vs Mwadui) na Mbeya (Mbeya City FC vs Prisons) huku Simba na Yanga zikitenganishwa katika raundi mbili zilizopita.
Na katika kile ambacho hatukubaliani nacho kutokana na mazingira ambayo tunaona yanaweza kusababisha upangaji wa matokeo, ratiba ya Kombe la FA haipangwi kwenye mazingira yanayoonekana wazi kwa umma. Imekuwa ikipangwa 'mafichoni' na maofisa wa TFF bila kushuhudiwa na vyombo vya habari.
Kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya soka la Tanzania na taifa kwa ujumla, tunaona mamlaka ya soka nchini (TFF) imeboronga na huenda, hatutapata mwakilishi sahihi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho brani Afrika mwakani.
Tunaendelea kulishauri shirikisho kuzingatia weledi na kuhakikisha michuano hiyo inaendeshwa kwa misingi sahihi ya soka kuanzia kwenye upangaji wa ratiba hadi usimamizi wa mechi zenyewe.
Tunaamini kuwa bila kuzingatia weledi na misingi sahihi ya kuendesha mashindano kwa mtindo wa mtoano, michuano ya Kombe la FA haitakuwa na tija yoyote kwa maendeleo ya soka nchini.
Na katika kupambana na kadhia ya upangaji matokeo ya mechi za soka ambayo imekithiri nchini, tulitegemea kuona TFF wanakuwa mstari wa mbele kuipiga vita kwa kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika kuchezesha droo na upangaji wa ratiba ya mashindano wanayoyasimamia,
lakini imekuwa kinyume chake. Ndiyo maana tunaona si busara kwa TFF kutumia maofisa wake wachache kuchezesha droo na kupanga ratiba ya robo-fainali ya Kombe la FA msimu huu wakiwa 'mafichoni' kwa manufaa ya shirikisho badala ya kuzingatia maslahi ya soka la Tanzania na maendeleo ya taifa.










