Migogoro ya uchaguzi imalizwe wananchi wapate maendeleo

03Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Migogoro ya uchaguzi imalizwe wananchi wapate maendeleo

HALMASHAURI kadhaa nchini, zimeingia katika migogoro ya kisiasa, baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Migogoro hiyo imesababishwa na uchaguzi wa wenyeviti na mameya wa halmashauri hizo na unakihusisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hadi sasa uchaguzi wa meya na makamu wake umeshindikana kufanyika katika Jiji la Dar es Salaam kutokana na mvutano ambao umesababisha uahirishwe mara kadhaa.

Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Jumamosi iliyopita, lakini katika mazingira ya kutatanisha, ilidaiwa kwamba kuna zuio la Mahakama, ingawa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekana kutoa amri ya zuio la mkutano huo kwa siku hiyo.

Utata huo ulisababisha vurugu kutokana na wajumbe wa Ukawa kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi huo na kusababisha vyombo vya dola kuingilia kati kuwadhibiti.

Jiji la Tanga licha ya kupata meya ambaye anatoka CCM, lakini umezuka mgogoro mkubwa kutokana na madiwani wa Ukawa kupinga matokeo hayo wakidai kuwa mgombea wa CUF ndiye aliyeshinda. Mgogoro huo umesababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo za Jiji hilo.

Hata Serikali imesema Halmashauri ya Jiji la Tanga itavunjwa kama wazee wa Tanga na viongozi watashindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nafasi ya Meya unaoikabili halmashauri hiyo.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi wa mkoa katika Ikulu ndogo ya jijini Tanga.

Madiwani wa upinzani walitangaza kutoshiriki kwenye vikao vya halmashauri hiyo na shughuli zozote za maendeleo kwa kile walichodai hawakutendewa haki katika uchaguzi wa meya wa jiji hilo.

Hali hiyo ilimshtua Makamu wa Rais, Samia wakati wa ziara yake mkoani Tanga na kutishia kuwa ikiwa mgogoro huo utaendelea, serikali itaivunja halmashauri hiyo kwa kuwa hakuna fedha za kurudia uchaguzi huo.

Pia Ukawa na CCM walivutana katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero ambayo inaundwa na majimbo mawili ya Kilombero na Mlimba.

Hata hivyo, uchaguzi huo ulifanyika juzi baada ya kuahirishwa kutokana na mvutano wa wajumbe halali wa kupigakura na CCM yenye madiwani 18 kuishinda Ukawa yenye madiwani 19. Uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira ya vurugu na Jeshi la Polisi kuwashikilia wabunge wawili wa Ukawa na madiwani kadhaa.

Matukio haya yote yanaonyesha kwamba lipo tatizo la msingi ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi. Kwanza, uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ufanyike katika mazingira rafiki yasiyo na mizengwe. Pili madiwani katika halmashauri zote waanze kuchapa kazi za kusimamia miradi kuwaletea wananchi maendeleo.

Wananchi baada ya kutekeleza jukumu lao la msingi la kikatiba la kuwachagua viongozi wao mwaka jana, wanachosubiri kutoka kwao ni kuwahudumia na kusimamia miradi ya maendeleo ili wapate maendeleo na siyo masuala ya itikadi za vyama.

Tunapaswa kuwa na kumbukumbu jinsi migogoro ya kisiasa katika halmashauri kadhaa nchini huko nyuma ilivyokwamisha maendeleo ya wananchi.

Migogoro ya kisiasa katika Jiji la Arusha na Manispaa ya Bukoba ilisimamisha shughuli za maendeleo ukiwamo utekelezaji wa miradi ya mamilioni ya fedha kwa zaidi ya miaka mitano baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kuwaathiri zaidi wananchi ambao maisha yao yanazitegemea halmashauri kwa kiwango kikubwa.

Tunaishauri Ofisi ya Rais (Tamisemi) kumaliza migogoro hii haraka na kwa kutenda haki ili wananchi wahudumiwe pamoja na kujenga imani ya wananchi kwamba serikali ya awamu ya tano inaheshimu na kufuata utawala bora.