Matokeo 8-0, 7-0 Ligi Daraja la 1 yakumbushe kanuni Usajili wa Klabu

22Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Matokeo 8-0, 7-0 Ligi Daraja la 1 yakumbushe kanuni Usajili wa Klabu
  • DONDOO MUHIMU: Hata kupanda daraja kwa Ruvu Shooting ni ukiukwaji wa kanuni za ligi za TFF toleo la 2015 kwa kuwa timu hiyo inamilikiwa na taasisi (JKT) ambayo tayari ina timu nyingine mbili Ligi Kuu (Mgambo JKT na JKT Ruvu).

JUNI 8-12, mwaka jana, Nipashe ilichapisha ripoti maalum iliyofichua jinsi upangaji matokeo ya mechi za soka unavyofanyika na athari za kadhia hiyo kwa maendeleo ya taifa.

Siku 12 baadaye, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipitisha kanuni mpya za ligi toleo la 2015 likiongeza adhabu ya faini isiyopungua Sh. milioni 10 kwa wapangaji matokeo.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa mwaka huu wa soka, shirikisho hilo halijamwadhibu mtu yeyote kutokana na makosa ya rushwa na upangaji matokeo licha ya vitendo hivyo kudaiwa kuota mizizi katika ligi mbalimbali za soka nchini.

Na wiki iliyopita TFF ikitangaza kuzifikisha mbele ya kamati yake ya nidhamu timu za Polisi Tabora, Oljoro JKT, Geita Gofd na JKT Kanembwa kutokana na kile ilichoeleza kuwa imebaini viashiria vya upangaji matokeo katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu kabla ya kuanika timu itakayopanda Ligi Kuu kutoka Kundi C.

JKT Kanembwa ilifungwa nyumbani mabao 8-0 dhidi ya Geita Gold FC mkoani Kigoma wakati Polisi Tabora iliichapa JKT Oljoro magoli 7-0 mjini Tabora.

Matokeo hayo yalizifanya timu zote zifunge msimu wa FDL zikiwa na pointi 33 kila moja baada ya michezo yote 15, lakini Geita inayofundishwa na Suleiman Matola ikaongoza kundi hilo kwa wastani mabao kabla ya TFF kuamua kuyasitisha.

Kabla ya mechi hizo, hapakuwa na timu nyingine yoyote iliyofungwa mabao kuanzia matano katika mechi moja mbali na kipigo cha 5-1 ilichokipata Mji Mkuu dhidi ya Friends Rangers Februari 7, mwaka huu.

Wakati TFF ikisaka ukweli wa vipigo vikubwa vya 8-0 na 7-0, binafsi ninafikiri ipo haja kwa shirikisho hilo lenye mamlaka ya soka nchini kuhakikisha linaisimamia vizuri kanuni ya Usajili wa Klabu (Club Licensing) liliyoiingiza kwenye katiba yake wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama wa TFF uliofanyika mjini Morogoro Machi mwaka juzi.

Ikumbukwe kuwa kati ya timu zote 24 zilizoshiriki FDL msimu huu, tano ni za Jeshi la Polisi (Polisi Tabora, Polisi Dar, Polisi Morogoro, Polisi Dodoma na Polisi Mara), nne za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambazo ni Ruvu Shooting, JKT Mlale, JKT Kanembwa na JKT Oljoro wakati Rhino Rangers ikiwa ni timu nyingine ya taasisi ya jeshi (JWTZ).

Binafsi ninafikiri katika mazingira haya, inakuwa ngumu kuukwepa upangaji wa matokeo kwa sababu timu nyingi zinatoka taasisi moja, tena ya kijeshi ambako 'kuna amri moja tu - ukiambiwa pia, ni lazima upige'.

Kadri ya uelewa wangu wa soka, hata kupanda daraja kwa Ruvu Shooting ni ukiukwaji wa kanuni za ligi za TFF toleo la 2015 kwa kuwa timu hiyo inamilikiwa na taasisi ambayo tayari ina timu nyingine mbili Ligi Kuu (Mgambo JKT na JKT Ruvu).

TFF ilipaswa kuweka wazi kwamba Ruvu Shooting itashiriki Ligi Kuu msimu ujao ikiwa tu JKT Ruvu na Mgambo JKT zitaporomoka daraja msimu huu.

Bila kuwa na utashi wa kutimiza matakwa ya kanuni za ligi, ninaamini soka la Tanzania litaendelea kutafunwa na kadhia ya upangaji matokeo kama ambavyo TFF wamehisi kujitokeza katika mechi za mwisho za Kundi C la FDL msimu huu.