Mchezo huo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua kutokana na timu hizo zote kuwa katika mbio za ubingwa.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana limetaja waamuzi watakaochezesha mechi hiyo, wote wakiwa na beji za Shirikisho la Soka Tanzania (FIFA), ambao ni Jonesia Rukyaa wa Kagera, atakayesaidiwa na Josephat Bulali wa Tanga, Samuel Mpenzu wa Arusha, wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Elly Sasii wa Dar es Salaam na Kamisaa atakuwa Khalid Bitebo wa Mwanza.
Simba na Yanga zinakutana Jumamosi katika mchezo wa sura tofauti kidogo na michezo mingi ya miaka ya miaka miwili iliyopita, safari hii ikionekana kuwa mechi ya ushindani zaidi.
Udhaifu wa miaka ya karibuni wa kikosi cha Simba uliifanya mechi ya watani wa jadi ipungue ladha, kwa sababu mara kadhaa imekuwa ikikutana na Yanga ikiwa haina inachogombea kwenye Ligi Kuu.
Kwa sasa Simba SC wanakwenda kukutana na Yanga SC wakiwa wao ndiyo wanaongoza Ligi Kuu iliyo katika mzunguko wake wa pili, kwa pointi zao 45 dhidi ya 42 za mahasimu wao hao ambao pia ni mabingwa watetezi.
Simba SC itataka ushindi Jumamosi ili kuendelea kukaa kileleni na kuweka hai matumaini ya kutwaa taji la kwanza la ubingwa wa Ligi Kuu tangu 2011, wakati Yanga SC nao wataingia uwanjani mwishoni mwa wiki kujaribu kuwaengua kileleni mahasimu wao.
Mapema tu inajionyesha ni kasi gani mchezo wa Jumamosi umeteka hisia za wengi kutokana na kuwa na picha tofauti na mechi kadhaa zilizopita.
Kwa uzito wa mchezo huo, Lete Raha tunachukua fursa kuwaambia TFF na bodi nyingine zote zinazohusika kwa namna moja au nyingine katika mchezo huo, kuhakikisha mazingira mazuri, salama na yenye kuridhisha kwa pande zote.
Tumepokea majina ya waamuzi; Jonesia Rukyaa, Josephat Bulali, Samuel Mpenzu na Elly Sasii, pamoja na Kamisaa Khalid Bitebo na tunaungana na TFF kwa sababu wote ni marefa bora kwa sasa nchini.
Kumbukumbu zinaonyesha katika mechi zilizopita waliwahi kufanya makosa ya kibinadamu, lakini tunaamini kwa uzoefu walioendelea kuupata, wamezidi kuiva.
Jambo muhimu Lete Raha tunapenda kuwaasa marefa hao ni kuhakikisha wanachezesha kwa mwongozo wa sheria 17 za soka, pasipo kuyumbishwa na mapenzi, chuki, jazba au rushwa.
Lete Raha tunaamini idara nyingine zote zikiwamo za ulinzi na usalama katika mchezo huo zinaweza kujikuta hazina kazi, iwapo marefa hao watachezesha kwa haki, bila kupendelea wala kuonewa upande wowote.
Maelfu watakaomiminika kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi watapenda kuona burudani safi na uchezeshaji wa haki, ili matokeo yawaridhishwe wengi.
Pamoja na hayo, tumeshuhudia vitendo visivyo vya kiungwana katika mechi za watani, ikiwamo mashabiki wa timu nyingine kupita katika jukwaa la wapinzani wao, iwe kwa bahati mbaya au kusudi.
Lete Raha tunaona haya si mambo ya kuendekezwa na lazima uwepo utaratibu wa kuhakikisha hayaendeli kutokea.
Mashabiki wapewe mwongozo wanapoingia tu milangoni kwa usalama wao wapitie wapi na waende kukaa wapi, ili kuhakikisha mashabiki hawapigwi tena. Lete Raha tunapenda kuona watu wanakwenda kufurahia mchezo Jumamosi na ndiyo maana tunawaambia TFF, tunataka mchezo safi wa haki bila upendeleo Simba na Yanga Jumamosi uwanja wa Taifa.










