Alisema kutokana na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano duniani, biashara ya simu na posta hivi sasa ina ushindani mkubwa unaohitaji mtazamo mpana wa kibiashara ili kukidhi mahitaji ya soko.
“Serikali inajitahidi kuzisaidia TTCL na Posta, hivyo wekezeni vizuri kwenye data na uharaka wa utoaji huduma ili mshindane kwenye soko na kukuza uchumi wa taasisi hizi muhimu kwa ustawi wa nchi,” alisema Profesa Mbarawa.
Kadhalika, alizitaka Menejimenti za Posta na TTCL kufanya kazi kwa uwazi na uadilifu ili malengo na mikakati ya taasisi hizo yafahamike kwa wafanyakazi wote na kuwezesha kujipima kama wanafikia malengo yaliyokusudiwa.
“Hakikisheni wafanyakazi wote wanaelewa malengo na mikakati ya tasisi zenu ili kazi ya kuyatekeleza ifanywe kwa umoja na ushirikiano”, alisema Profesa Mbarawa.
Aliongeza kuwa ndani ya TTCL na Posta, wapo baadhi ya watumishi wazembe, wavivu na wanaoihujumu serikali na kuonya kuwa wakibainika wataondolewa mara moja.
"Ni bora kubaki na wafanyakazi wachache waadilifu kuliko wengi wasiotimiza malengo," alisema.
Naye Meneja wa TTCL Mkoa wa Mwanza, Johnbosco Calista, alisema wigo wa mtandao kutofikia walaji wengi, wateja kutolipa madeni kwa wakati na ulinzi na usalama wa miundombinu ya mawasiliano, ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili shirika hilo mkoani humo.
Kwa upande wake, Meneja wa Posta Mkoa wa Mwanza, Julius Chifungo, alisema uchakavu wa barabara, maslahi yasiyokidhi ya wafanyakazi na uchakavu wa majengo, ni miongoni mwa vikwazo vinavyoathiri utendaji kazi wa shirika hilo mkoani humo.
Takriban masanduku 9,000 yanasimamiwa na Shirika la Posta mkoani Mwanza katika ofisi zake 11 na asilimia 96.8 hukodishwa na kuliingizia shirika hilo faida.
Aidha, kwa upande wa TTCL Mkoa wa Mwanza, inahudumia takriban wateja 45,041.










