Vitendo hivi vya uhalifu Dar vipatiwe suluhisho la kudumu

09Oct 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Vitendo hivi vya uhalifu Dar vipatiwe suluhisho la kudumu

VITENDO vya uhalifu jijini Dar es Salaam, vikiwamo vya uporaji wa mali kama vile simu, vito na fedha vimezidi kukithiri hadi kuonekana kuwa sawa na mfupa uliomshinda fisi.

Katika taarifa ya uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa wiki kadhaa, imebainika kuwa sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam, kumeibuka vikundi vya uporaji ambavyo vimekuwa vikitumia silaha mbalimbali kama viwembe, bisisisi, mapanga na nondo.

Kutokana na kuwapo kwa vitendo hivyo, mbali na kuibiwa, baadhi ya wananchi wamekuwa wakipata matatizo ikiwamo kuumizwa na hata kuipata ulemavu.

Baadhi ya maeneo ambayo yametwajwa kuhusika kwa kiwango kikubwa kwa matukio hayo ni Tazara, Msimbazi Centre, mabondwe ya Kigogo na Mkwajuni, Majumba sita njia panda ya Segerea, Mwenge, Kijitonyama, Tandale Kwa Mtogole, Chang’ombe na Mbagala.

Wakabaji na waporaji hao, ambao hujificha katika vichaka na majumba mabovu karibu na maeneo hayo, huwavamia wananchi wanaopita njia au walioko kwenye vyombo vya usafiri na kuwapora kisha kuondoka.

Wakati mwingine, wamekuwa wakipora mchana kweupe na kutembea kwa madaha bila kuchukuliwa hatua zozote.

Sambamba na hilo, vibaka hao wamekuwa wakivamia watu wanapoharibikiwa na magari kwenye barabara , ikiwamo ya Kawawa, nyakati za usiku na kuwapiga kisha kuwapora mali na kuharibu magari kwa kuiba vitu muhimu kama vioo na taa.

Kukithiri kwa uporaji na ukabaji huo kumesababisha hali ya Amani na usalama kwa wananchi kuwa shakani.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba watu badala ya kuwa na uhakika wa mali zao, wamekuwa na hofu hata wakiwa wanasafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Mambo kama hayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara ndani ya jiji la Dar es Salaam, yakiwemo yale ya vikundi hatari vinavyovamia makazi kama vile Komando Yoso, Kiboko Msheli na Mbwa Mwitu. Makundi hayo yalipoibuka na kufanya uhalifu, yalizimwa mara moja na hata baadhi ya wahusika kuuawa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Ni wazi kwamba vitendo hivyo vinavyofanywa sehemu kadhaa ambazo sasa zimeelezwa kuwa ni hatarishi, vinafahamika na mamlaka husika likiwamo Jeshi la Polisi lililopewa dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao.

Kutokana na ukweli huo, ni vyema hatua madhubuti zikachukuliwa ili kuifanya Dar es Salaam kuwa sehemu ya amani huku watu wake wakiishi kwa raha mustarehe dhidi ya vitendo viovu ambavyo ni tisdhio kwa amani na usalama.

Tunasema hivyo kwa sababu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alisema hivi karibuni kwamba wamejipanga kukabiliana na vitendo vyote vya kihalifu, vikiwamo vya uporaji na ukabaji.

Katika kukabiliana na vitendo hivyo, makonda alisema mkakati kabambe wa kupambana na uhalifu unahusisha kusogeza huduma za polisi maeneo yanatajwa kuwa hatari ambao umeshaanza kuzaa matunda kwa kukamatwa watu wanaodaikwa kuwa majambazi kwenye sehemu kadhaa ikiwamo ufukwe wa bahari wa Coco.

Mbali na operesheni hiyo inayohusisha doria ya magari na pikipiki, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, aliongeza kuwa mpango huo pia unahusisha uwapo wa vituo vya polisi vinavyohamishika kwenye maeneo ambayo hayana huduma hiyo.

Licha ya kuwapo mikakati hiyo, ni vyema ikawa endelevu badala ya kuwa ya mfumo wa zimamoto. Tunasema hivyo kwa sababu baadhi ya matukio yamekuwa yakitokea na polisi kuyapatia ufumbuzi lakini baada ya muda mfupi huibuka tena.

Pamoja na kazi hiyo kufanywa na polisi, ni vyema wakashiriki kikamilifu kwa kuanzisha ulinzi shirikishi

katika maeneo yanayoishi na pia kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa juu ya watu wanaoshiriki vitendo hivyo viovu, kwa sababu baadhi ya wahusika wanaishi kwenye maeneo ya makazi yao.