Simba iwaelimishe ustaarabu mashabiki wake

08Oct 2016
Mhariri
Nipashe
Simba iwaelimishe ustaarabu mashabiki wake

MWISHONI mwa wiki hii, klabu ya Simba imemwandikia barua Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kumuomba awaombee msamaha kwa Rais John Magufuli kutokana na uharibifu waliofanya mashabiki wake Uwanja wa Uwanja wa Taifa.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema kuwa wanalazimika kuomba radhi kutokana na ukweli kuwa, ingawa uwanjani kulikuwa na mashabiki wa Simba na Yanga, lakini ukweli wale wa Msimbazi ndiyo walihusika moja kwa moja na kung'oa viti vya uwanja huo na kusababisha hasara kubwa.

Kadhalika, mbali na kuomba msamaha, Simba pia wameiangukia Serikali itengua uamuzi wa kuwazuia kutumia uwanja huo.

Pia katika kuhakikisha mashabiki wakorofi wanadhibitiwa, wameiomba menejimenti ya uwanja kufunga kamera za ulinzi ili iwe rahisi kuwabaini mashabiki wasio na nidhamu.

Nipashe kama wadau wa soka, tunachukua nafasi hii kuipongeza klabu hiyo ya Msimbazi kwa kuonyesha uungwana na kukubali makosa.

Jamii yoyote inayolenga kuishi kistaarabu huwa ya kwanza kutambua makosa waliyofanya na kuomba radhi.

Ni kweli kitendo walichofanya mashabiki wa Simba siyo tu kwamba kimetoa taswira ya aibu mbele yao, lakini kimeitia hasara Serikali.

Ikumbukwe kuwa Uwanja wa Taifa ni miongoni mwa ile bora kabisa Afrika Mashariki na Kati.

Kutokana na ubora wake, Timu ya Taifa ya Brazil iliwahi kuja kucheza mchezo mmoja wakati ikiwa njiani kwenda kushiriki fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mara ya kwanza Afrika Kusini.

Kama uwanja huo usingekuwa bora, bila shata ingekuwa ndoto kwa timu kama Brazil kuja nchini.

Uwanja umetumia gharama kubwa ambazo ni kodi za wananchi wakiwamo mashabiki wenyewe waliovunja viti vya uwanja huo.
Hata hivyo, wakati Simba ikiomba msamaha kwa kitendo cha mashabiki wake kuharibu uwanja, ipo haja uongozi wa klabu hiyo kuelimisha mashabiki wake juu ya umuhimu wa kutunza uwanja huo.

Bila kutoa elimu kwa mashabiki hao, haitashangaza klabu hiyo siku nyingine tena kusimama mbele na kuomba radhi kutokana na tatizo kama lililotokea.

Tunasema hivyo kwa sababu, hii siyo mara ya kwanza mashabiki kuharibu miondombinu ya uwanja huo.

Ni sawa na mchezo unaojirudia mara kwa mara. Hivyo basi ni jukumu la klabu hiyo kuhakikisha vitendo hivyo havijirudii tena.
Mashabiki lazima wakubali kuwa mchezo wa soka unaendeshwa kwa sheria na taratibu zinazotambuliwa na mamlaka husika.

Kufanya vurugu, kuharibu mali na kuhatarisha usalama kwa sababu tu ya kutokukubaliana na uamuzi, ni ushabiki unaposwa kuepukwa.