Mama huyo mwenye watoto saba akizungumza na waandishi wa habari amesema mwezi Novemba mwaka 2023 alianza kujihisi ana ujauzito kwani alikuwa na dalili zote zinazoonesha kuwa yeye ni mjamzito japo alikuwa hajawahi kwenda kupima.
"Ilipofika mwezi wa kumi na moja mwaka jana nikaacha kuona siku zangu nikakaa sasa jana nikiwa nafunga biashara zangu usiku tumbo likaanza kuniuma nikajikaza kufika nyumbani likaendelea kuniuma sana nikawa nimemuita jirani yangu angalau aweze kunipeleka hospitali"
"Yule jirani yangu alipofika akanikuta niko katika harakati ya kusukuma akaniambia basi vua hizo nguo nikavua baada ya kusukuma mara moja mara mbili mara ya tatu ndio yakatoka yale majitu sasa akawa amemulika na tochi sasa akaona kale kandege kametanguliza mdomo na miguu kameweka hivi" ameeleza mwanamke huyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kigoma Road Zakaria Michael Joseph amesema alipopata taarifa za tukio hilo alifika eneo la tukio na kufanya jitihada za kumpeleka kituo cha afya Kasamwa kwa ajili ya uchunguzi.
"Tukio hili la mama kujifungua ndege nililipata majira ya saa tisa baada ya hapo tulifanya jitihada za kumfuatilia hatimaye tulimpata tukamchukua tukaelekea naye hospitali kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi" amesema Zakaria Michael ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigoma Road.
Hata hivyo Dk. Emmanuel Chalagela ambaye ni daktari kutoka kituo cha Afya Kasamwa anasema walivyomfanyia uchunguzi hawakuona dalili yoyote ya mama huyo kujifungua.
"Ni kweli mwanamke huyo tumempokea tulipomuhoji alisema alikuwa na miezi mitatu hajawahi kuona siku zake lakini alikuwa hajawahi kupima kuthibitisha ujauzito lakini pia tulivyompokea tulimfanyia uchunguzi wa kidaktari tulikuta njia yake ya uzazi imefunga na hakuna damu zinazoonesha dalili ya kujifungua tulienda mbali tukapima na kipimo cha mkojo na chenyewe kilionesha kabisa ni negative kwamba hakuwa na ujauzito" amesema Dk. Emmanuel Chalagela