Misaada yazidi kumiminika waathirika maporomoko Hanang’

05Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Misaada yazidi kumiminika waathirika maporomoko Hanang’

MISAADA kwa waathirika wa maporomoko ya tope wilayani Hanang’ inazidi kumiminika, hivi sasa vifaa vya ujenzi vya Sh. milioni 7.7 vimepokelewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Mkombozi, Respige Kimati (mwenye suti) akikabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi venye thamani ya kiasi cha sh.Milioni 7.7 kwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja. Picha: Mpiga Picha Wetu

Maporomoko hayo yalitokea Desemba 3 mwaka jana na kusababisha uhalibifu wa miundombinu, mali pamoja na maelfu ya wakazi wa mji wa Katesh kukosa sehemu ya kuishi.

 

Msaada huo umetolewa juzi na Benki ya Biashara ya Mkombozi na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja. pamoja na rangi za nyumba za mafuta na maji, (primer, solvent, red oxide, black paint), roller brush na hand brush.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo mkoani Manyara Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Respige Kimati alisema benki yao ni ya wananchi, ipo mbele katika kuhakikisha inatoa huduma mbalimbali za kibenki.

 

Alisema katika nyakati kama hizo wamekuwa wakiungana na Watanzania kuwashika mkono kama walivyofanya kwa wananchi wa Hanang’ kwa namna moja ama nyingine, kuwarudisha katika hali yao ya kawaida.

 

''Tunafurahi sana siku ya leo kukabidhi vifaa hivi kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya hii ya Hanang kama msaada wetu ili kwa utaratibu mliojiwekea uweze kuwafikia wale wote wananchi waliopata na maafa,''alisema.

 

Aliongeza: ''Tunatoa pole kwa wale waliopatwa na maafa ambao walipoteza ndugu na jamaa zao, Benki ya Mkombozi inatazama na kushughulika na wateja wa aina zote, tumeweka kipaumbele kwa wateja wadogo wadogo wakiwemo wa vijijini na kujenga mtandao ambao utaimarisha utoaji wao wa huduma za kibenki”

 

Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja alishukuru uongozi wa benki hiyo kwa kufika katika wilaya hiyo kwa kwenda kuwapa pole waathirika na kuwapatia vifaa vya ujenzi.

 

 

 

Alisema takribani nyumba 108 zinatarajia kuanza kujengwa ndani ya wiki hii, huku miundombinu mbalimbali ikiwa imekamilika katika eneo hilo la ujenzi ikiwemo maji, umeme pamoja na miundombinu ya barabara.

 

''Tunashukuru Mkombozi Benki kwa kutukimbilia kwa upendo wenu, Hanang inaendelea kurudi katika hali yake ya awali hatua kwa hatua, hivyo vifaa hivi tulivyopokea lengo lake kubwa ni kuongeza nguvu katika ujenzi huu wa nyumba,''alisema.

 

Aidha aliwasihi uongozi wa benki hiyo kuangalia namna ya kuwagusa wakulima, wafanyabiashara katika kuwainua kiuchumi.