Aidha, wananchi wametakiwa kuondokana na hofu ya kutembelea wafungwa magerezani kwa maelezo kuwa ni mahali salama ambapo mtu yeyote anaweza kutembelea na kuwasaidia wafungwa kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Wito huo umetolewa na Msaidizi wa Mkuu wa Gereza la Ruanda jijini Mbeya upande wa wanawake Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Enea Mwaisemba wakati akipokea mahitaji ya wafungwa wanawake yaliyotolewa na wadau.
Wadau waliotoa misaada hiyo ni Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Sauti ya Mama Afrika kwa kushirikiana na Taasisi ya Twende Pamoja ambazo zinashughulikia mambo mbalimbali ya kijamii mkoani Mbeya.
Mwaisemba amesema licha ya jitihada za serikali kuhakikisha wafungwa wanapata huduma zote, lakini wanahitaji ushirikiano kutoka kwa jamii kusaidia mahitaji mengine kwa wafungwa hao hasa wanawake kwa kuwa wanao uhitaji mkubwa.
“Nawashukuru sana kwa kuleta mahitaji haya, niwaombe tusisubiri wakati wa sikukuu na matukio maalumu tu ndipo tulete msaada gerezani, watu wetu wanayo mahitaji wakati wote hivyo kila mnapofanikiwa njooni mara kwa mara,” amesema.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Sauti ya Mama Afrika, Tabitha Bugali, amesema wameshirikiana na Taasisi ya Twende pamoja Foundation kutoa vitu vyenye thamani ya zaidi ya Sh. 480,000, ikiwa ni sehemu ya kuwapa faraja wafungwa wanawake kuelekea kilele cha Siku ya Mwanamke Duniani Machi 8.
Amesema wametoa mahitaji mbalimbali ikiwamo taulo za kike, sabuni, mafuta ya kupaka, miswaki, dawa za meno pamoja na mavazi ili kuwasitiri wanawake wenzao.
Amewataka wadau na taasisi zingine za kijamii kushirikiana na serikali kuwasaidia wafungwa hao akieleza kuwa gerezani ni sehemu ya kurekebisha tabia na siyo sehemu ya mateso kama ambavyo wengi wamekuwa wakifikiri.
“Tumeona tujumuike na wenzetu kuwapa faraja ili wasione kama wameadhibiwa, kwa sababu kwa sasa tunajua magereza ni chuo cha mafunzo ili wanapotoka hapa wakawe raia wema,” amesema Tabitha.
Hata hivyo amesema wataendelea kuwatembelea wafungwa hao pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii wakiwamo watoto yatima kwa lengo la kuyafariji.
Machi 8 ya kila mwaka wanawake nchini wanaungana na wenzao duniani kote kuadhimisha siku yao kwa lengo la kutetea haki zao na kuhamasishana kuchangamkia fursa mbalimbali zikiwamo kuwania nafasi za uongozi serikalini.









