Watu 15 wafariki dunia ajali ya Lori na magari matatu Arusha

25Feb 2024
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Watu 15 wafariki dunia ajali ya Lori na magari matatu Arusha

WATU 15 wamefariki baada ya lori la mizigo lililokua linatoka mpakani Namanga kuja Arusha Mjini kufeli breki na kugonga Coster ya Shule,Haice na gari la mtu binafsi 

Akizungumza katika Hospitali Mkoa Mount Meru wakati miili ya ajali hiyo ikipelekwa kuhifadhiwa,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Justine Masejo alisema  ajali hiyo ilitokea Februari 24 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni eneo la Kibaoni Ngaramtoni wilayani Arumeru.

 

"Miili imehifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa Mount Meru na majeruhi wapo kadhaa ambao wamelazwa Hospitali hiyo na wengine Selian,"alisema.

 

Alisema halo za majeruhi ni mbaya na madaktari wanaendela kuwapatia matibabu.

 

Mashuhuda wa ajali hiyo, Anthony Laizer alisema amesikitishwa kuona baadhi ya vijana badala yabkusaidia kuokoa majeruhi wanakimbilia kupekua mizigo ya wahanga wa ajali hiyo kutafuta vitu vya thamani na fedha.

 

"Kweli naomba wazazi tuzungumze na vijana wetu hali ya malezi sio nzuri nimesikitika sana na tabia hii tuiache,"alisema.

 

Naye Amina Salum alisema kwa macho yake ameona baadhi ya vijana wakipelua maiti za watu kwenye mifuko kutafuta fedha na kuachia wazee wakibeba miili hiyo.

 

Alisema  baadhi wakipekua mizigo ya waliopata ajali wa coaster ya Shule ya New Vision,hali hiyo siyo utamaduni wa Tanzania na mbaya sana.

 

Aidha alisema pia Taifa inabidi litafutiwe ufumbuzi wa tabia za watu kupiga picha viungo vya watu vilivyotapakaa barabarani kwa simu za kiganjani 

 

"Naomba watu wa namna hii wakirusha mitandaoni picha hizi wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.Yaani mtu badala ya kukimbilia kuokoa mtu anapiga picha sio utu,"alisema.