Misamaha ya wagonjwa yagharimu mabilioni MNH

23Feb 2024
Pilly Kigome
Nipashe
Misamaha ya wagonjwa yagharimu mabilioni MNH

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema kwa mwaka imekuwa ikipoteza kati ya Sh. bilioni 17 hadi Sh. bilioni 20 kutokana na misamaha inayotolewa kwa wagonjwa wanaoshindwa kulipia gharama za matibabu.

Mabilioni hayo yamekuwa yakitumika kwa wagonjwa wanaosamehewa wakati wanaruhusiwa kurudi nyumbani wakiwamo waliofariki dunia hospitalini hapo wakati wakitibiwa.

Katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu tayari hospitali hiyo imepoteza Sh. bilioni 3.5 katika kutoa misamaha hiyo.

Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Huduma wa MNH, Dk. Samson Ndile, alisema jana hospitalini hapa wakati akiwa katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Dk. Ndile alitoa takwimu hiyo baada ya kutakiwa kujibu tuhuma na malalamiko kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Kinondoni waliokuwa wakilalamika kuwa wanazuiliwa kuchukua maiti zao kutokana na kushindwa kulipa gharama za matibabu za wapendwa wao.

Dk. Ndile alisema hakuna mtu ambaye amezuiwa kuchukua maiti bali kinachotokea ni watu kutaka wapewe misamaha bila kufuata taratibu stahiki.

Akieleza utaratibu unaotakiwa, Mkurugenzi huyo alisema kwa mwananchi aliyeshindwa kulipia gharama hizo hutakiwa kwende katika Ofisi ya Ustawi wa Jamii hospitalini hapo akiwa na barua iliyothibitisha ukaazi kutoka katika Ofisi za Serikali ya Mtaa anakoishi kupitia kwa Mkurugenzi wa hospitali.

Alisema ikithibitika anahitaji msamaha basi uongozi unatoa msamaha bila kipingamizi chochote.

“Hatuwezi kuruhusu mgonjwa aliyeshindwa kulipa gharama au kutoa maiti kiholela bila utaratibu wananchi wanatakiwa waelewe hivyo.

“Kufanya hivyo kunawarahisishia (wao) kutoa maelezo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pindi anapokuja kukagua mahesabu hospitalini hapo,” alisema.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mwananyamala Mwinjuma, Kata ya Makumbusho, Mtaa wa Kichangani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alitoa siku saba kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) warudishe maji.

Chalamila alitoa agizo hilo kutokana na kilio kikubwa cha wananchi cha ukosefu wa maji wa zaidi ya wiki moja sasa.

Akitolea ufafanuzi kuhusu tatizo la kukatika maji, Kaimu Meneja wa DAWASA Kinondoni, Frank Sulley, alisema kuwa, ukosefu huo wa maji jimboni humo unasababishwa na kukatika kwa umeme na kuharibika kwa miundombinu ya mifumo ya maji baada ya mvua.

Sulley alitaja maeneo yaliyoathirika zaidi ni Kijitonyama, Ali Maua A na B, Masaki Mwisho na Mmananyamala Kisiwani. Katika mkutano huo wananchi walilalamika kukosa maji zaidi ya wiki sasa.