Mjane vipande nyama swala aachiwa huru

17Feb 2024
Francis Godwin
Iringa
Nipashe
Mjane vipande nyama swala aachiwa huru

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, imemwachia huru Maria Ngoda, mkazi wa Isakalilo wilayani Iringa, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 22 jela kwa hatia ya kukutwa na vipande 22 vya nyama ya swala.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Elvin Mgeta, baada ya kukubaliana na hoja zilizowasilishwa na mkata rufani na kutamka kuwa hana hatia na yuko huru.

Ngoda alipandishwa kizimbani jana majira ya saa 6:29 mchana kusomewa hukumu ya rufani yake iliyosajiliwa na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).

Awali, Ngoda  alihukumiwa kifungo cha miaka 22 Novemba 3, 2023 na Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Said Mkasiwa, baada ya kumtia hatiani.

Kutolewa kwa hukumu hiyo kuliibua mjadala kutokana na kidhibiti kilichodaiwa kuwa alikutwa nacho na idadi ya miaka aliyohukumiwa, hivyo ilisababisha makundi mbalimbali kupaza sauti, huku baadhi wakitangaza kumpa msaada wa kisheria kukata rufani.

Baada ya kutolewa kwa hukumu iliyomweka huyu, Ngoda alisema: "Asante Mungu, nawashukuru ndugu zangu kunipigania. Mimi  ni mama mjane na wanangu kwa kipindi hiki chote sijui walikuwa katika hali gani. Asante Mungu."

Pia alionekana akibubujikwa na machozi muda wote huku akiwashukuru wote waliomsaidia katika rufani yake.

Akisoma hukumu kwa dakika 42, Jaji Mgeta alikubaliana na hoja 13 za wakata rufani ikiwemo ya ushahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kosa pasipo kuacha shaka yoyote.

Jaji Mgeta alisema hoja zilizo wasilishwa na upande wa warufani zina mashiko ikiwamo suala la Ngoda kukosa uwakilishi wa kisheria wakati kesi yake ya awali inaendeshwa, huku upande wa mashtaka ukiwa na mawakili sita.

Hoja nyingine ni uthibitisho kama vipande vya nyama alivyokutwa navyo ni vya nyama pori, kwa maana ya swala kama ilivyodaiwa au la.

"Alipotoa ushahidi mtaalamu wa nyama pori alisema ana uhakika wa nyama hiyo kuwa ya swala kwani mbavu za nyama ya pori ni nene tofauti na mnyama wa kufugwa, japo hakusema ni mnyama yupi anayemfananisha naye. Ila  ni ukweli kuwa mbavu za ng'ombe ni kubwa kuliko za swala wakati ng'ombe si mnyama pori, hivyo ushahidi huo hauna mashiko" alisema Jaji Mgeta.

Pia Jaji Mgeta alisema hakukuwa na mnyororo mzuri wa utunzaji wa nyama ambayo inadaiwa kukutwa kwenye ndoo aliyokutwa nayo Ngoda 

Hoja nyingine ni suala la Ngoda kutosikilizwa ushahidi wake kwamba nyama ile alikuwa amekabidhiwa na mtu aliyedai kwenda kufuata hela.

"Suala la Maria  (Ngoda) kukutwa kwenye eneo la tukio na ndoo ambayo ilidaiwa kuwa na nyama ni vitu viwili tofauti. Maria alikataa ndoo si yake na utetezi huo ulipuuzwa,” alisema.

Jaji Mgeta alisema kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha utetezi wao, mahakama hiyo inafuta kesi hiyo na kumwachia huru mshtakiwa.

Alisema endapo upande wa mashtaka hautaridhika na hukumu hiyo, unaruhusiwa kukata rufani ndani ya siku 30 kuanzia Februari 16, mwaka huu.

NJE YA MAHAKAMANje ya viwanja vya mahakama idadi kubwa ya wananchi walijitokeza kufuatilia, kusikiliza kesi hiyo, wakiwamo wanawake.

Wakili wa TLS, Laetitia Ntagazwa, akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama baada ya hukumu hiyo alisema Mahakama Kuu imetenda haki.

Alisema wakati wote wa kesi TLS imejitolea bure kumtetea mjane huyo na hakuna pesa yoyote iliyotozwa, hivyo alitoa wito kwa watu wenye changamoto ya msaada wa kisheria na hawana uwezo wa kufungua kesi wala kuwalipa wanasheria wafike katika ofisi za TLS kwa msaada.