Chanjo surua rubella kunusuru maisha ya watoto ZAIDI ya 109 Chato

09Feb 2024
Daniel Limbe
Chato
Nipashe
Chanjo surua rubella kunusuru maisha ya watoto ZAIDI ya 109 Chato

KUTOKANA na uwepo wa tishio la ugonjwa wa surua kwa baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita,serikali imeweka mpango kabambe wa kutoa chanjo ya surua rubella kwa lengo la kudhibiti ugonjwa huo kuenea maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Aidha watoto wote wenye umri kuanzia miezi tisa na wale walio chini ya miaka mitano wanatarajiwa kunufaika na mpango huo.

Mratibu wa chanjo wilaya hiyo,Melkizedeck Kimario,amesema wilaya hiyo inakusudia kuwafikia zaidi ya watoto 109,384 na kwamba ili mpango huo ufanikiwe ipo haja kwa jamii,viongozi wa dini,siasa,makundi maalumu na taasisi mbalimbali kuielimisha jamii umuhimu wa chanjo ya Surua rubella kabla ya mpango huo kuanza kutekelezwa Februari 15 hadi 18 mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Chato,Mhandisi Deusdedith Katwale,ametaka maazimio ya wajumbe wa kamati hiyo kusimamiwa na kutekelezwa haraka kabla ya zoezi hilo kuanza ikiwemo kutoa walaka maalumu kwa viongozi wa madhehebu ya dini utakaosomwa makanisani, mikutano ya vijiji na vitongoji pamoja na kuwashirikisha waganga wa tiba za Jadi kusaidia kupaza sauti zao ili mpango huo uweze kuonyesha matokeo yanayokusudiwa kwa manufaa ya ustawi wa jamii.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chato,Dk. Halifa Mshana, amesema mpango huo unatarajiwa kutekelezwa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwafikia walengwa majumbani (huduma mkoba), kwenye vituo vya kutolea huduma za tiba na kwamba jamii haina sababu ya kuogopa kujitokeza kwa kuwa chanjo hiyo haina madhara kwa binadamu na kwamba imelenga kudhibiti vifo visivyokuwa vya lazima kwa jamii.

Uamuzi huo wa serikali umekuja baada ya mwaka jana wilaya ya Chato kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Surua ambapo watoto zaidi ya 28422 sawa na aslimia 115 ya lengo walifikiwa na kuchanjwa.