Mrisho: Gati zote zinafanya kazi na meli zinaendelea kupokelewa

28Jan 2024
Beatrice Shayo
Nipashe Jumapili
Mrisho: Gati zote zinafanya kazi na meli zinaendelea kupokelewa

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho, amesema gati zote zinafanya kazi na kwa sasa meli zinaendelea kuhudumiwa katika maeneo hayo.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho.

Mrisho aliyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa ufafanuzi kuhusu madai ya uwepo wa msongamano bandarini kutokana na kutofanya kazi kwa baadhi ya gati. 

"Gati zote zinafanya kazi na meli zinaendelea kupokelewa kwa leo pekee kuna meli 13 kwenye gati zote kuanzia gati namba 0 hadi gati 11 zikiendelea kuhudumiwa na meli 31 zikiwa zinasubiri kuhudumiwa," amesema Mrisho.

Mrisho amesema upande wa gati za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), terminal l kuna meli 10 zikiendelea kuhudumiwa ambazo zimebeba shehena mbalimbali 

"Pale gati namba 0 kuna meli ya MV Yangze 32 inapakua, gati namba moja kuna meli ya MV Loa Fortune inahudumiwa, gati namba mbili kuna MV African Macaw, huku gati namba tatu kukiwa kuna meli ya MV Tong Da na meli zote hizi zinapakua mizigo mchanganyiko" amesema na kuongeza kuwa;

"Gati namba nne hivi sasa kuna meli ya MV Fearless, gati namba tano kuna MV Anassa, gati namba sita  na saba kuna MV MSC Nora III, pale KOJ I kuna meli ya MT NCC Abha, KOJ II kuna meli ya MT Lubersac na mwisho pale SPM kuna meli ya MT Torm Hannah ikiendelea kupakua" 

Mrisho amesema katika gati za TPA terminal ll, ambazo ni gati namba nane hadi 11 hivi sasa kuna meli tatu zikiendelea kuhudumiwa.

Ufafanuzi huo umetolewa, kutokana na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa kuna gati mbili pekee ndio zinazofanya kazi katika bandari ya Dar es Salaam. 

Kukamilika kwa sehemu ya miradi ya maboresho ya miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam kumeanza kuleta matokeo chanya na kuongezeka kwa idadi ya shehena bandarini.