Wauza sukari Chato wapuuza agizo la serikali

25Jan 2024
Daniel Limbe
CHATO
Nipashe
Wauza sukari Chato wapuuza agizo la serikali

LICHA ya serikali kutoa bei elekezi kwa wafanyabiashara wa sukari nchini, agizo hilo limeonekana kupuuzwa wilayani Chato mkoani Geita kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuuza kwa bei ya kinyonyaji kwa lengo la kujipatia faida mara dufu, huku wananchi wakiomuomba Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe-

-kufika wilayani humo kujionea mwenyewe.

Nipashe Digital imezungukia baadhi ya wafanyabiashara wadogo wa sukari na kubaini sukari kilo moja kuuzwa kwa shilingi 3800, 3900 hadi 4,000 kwa ile ya pakiti na kwamba bei hizo zinatokana na kupanda kwa sukari kiwandani jambo linalopingwa na wananchi.

Leonia Stephano na Juma Hamad, wamesema ipo haja kwa serikali kuingilia kati bei hizo ikiwa ni pamoja na kuwakamata wale wote wanaokiuka bei elekezi ya serikali kwa lengo la kujipatia faida kubwa pasipo kutazama maumivu wanayopata wananchi wa chini.

Kwa mujibu wa Wakala wa Sukari ya Kagera (Kagera Sugar) aliyepo mjini Chato, Marco Madirisha amesema bei ya jumla kwa mfuko mmoja wenye ujazo wa kg 50 ni shilingi 90,000.

Hata hivyo serikali kupitia taarifa rasmi ya Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Sukari nchini, Kenneth Bengesi, inaelekeza bei ya kilo moja ya sukari kwa mikoa ya kanda ya ziwa ikiwemo Mwanza, Mara, Shinyanga, Geita iuzwe kati ya shilingi 2,800 hadi 3,000 na si vinginevyo.