W’biashara walalamika mitaro kutosafishwa

04Jan 2024
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
W’biashara walalamika mitaro kutosafishwa

BAADHI ya wafanyabiashara katika Mtaa wa Lumumba, jijini Mwanza wamelalamikia tatizo la mitaro ya barabara kujaa taka na kuziba wakati mvua inaponyesha na kuingia katika maeneo yao ya biashara.

Walitoa kilio chao wakati wakizungumza na Nipashe adha wanayoipata mvua iliponyesha kwa muda wa robo saa na kusababisha maji kutuama barabarani na maeneo ya biashara zao.

Mmoja wa wafanyabiashara, Abdalah Madege alisema chanzo cha maji kutuama ni taka zinazotupwa katika mitaro ya barabara zikiwamo chupa na kushindwa kuruhusu maji kupita.

“Maji yanaingia hadi ndani ya maduka na kusababisha kulowanisha bidhaa zetu na kukosa kabisa soko kwani huwa zinaharibika na kutusababishia hasara tumelalamika sana juu ya suala hili, lakini bado halijapatiwa ufumbuzi,” alisema Madege.

Wilfred Minani, mfanyabiashara mwingine wa eneo hilo, aliiomba serikali kudhibiti uchafuzi huo kwa kuweka utaratibu wa kusafisha mitaro hiyo kwa kuwa wanalipia fedha za usafi, lakini hawaoni utekelezaji wake.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati, amekiri kuwapo kwa adha hiyo na kuwaomba wamiliki wa nyumba za biashara kuzifanyia marekebisho ili ziwe imara.

“Tayari tumewasilisha tatizo hili la mitaro serikalini ili ifanyie marekebisho ya kudumu katika miundombinu inayozunguka maeneo ya wafanyabiashara na kuondoa hasara za mara kwa mara zinazowakabili wafanyabiashara wote,” alisema Masagati.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla akizungumza katika kikao cha bodi ya barabara mkoani hapa, aliwaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi pamoja na wenyeviti wa halmashauri kuweka utaratibu wa muda mrefu wa kudhibiti uchafuzi katika mitaro ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuizubua kila mara kwa kushirikiana na wananchi.

Alisema kazi hiyo haitakiwi kutelekezwa kwa TARURA na TANROADs kwa sababu wana majukumu mengine ya kuhakikisha wanapanua na kuongeza miundombinu na kwamba sio vyema kutumia muda mrefu katika kukabiliana na kuziba kwa mitaro.