Ni manusura wa maporomoko ya tope, mawe na magogo kutoka Mlima Hanang, mkoani Manyara na kuua watu 89, kujeruhi 116, Paula Neema, akisimulia kilichotokea siku hiyo akiwa na watoto wake 11 ndani ya nyumba.
Anasema anaona ni kama ndoto yeye na familia yake ya watoto hao kuwa wazima hadi sasa.
Maafa hayo yalitokea usiku wa Desemba 3, mwaka huu, baada ya mlima huo uliokuwa umenyonya maji mengi yaliyotokana na mvua kubwa kumeguka na kuanza kuporomosha tope zito na magogo kwenye nyumba zilizopo karibu.
Paula Mkazi wa Kijiji cha Gendabi, alisema wakati wa tukio hilo Mungu alimpa nguvu na ujasiri wa kuiokoa familia yake na kufanikiwa kuwakimbiza kuelekea eneo la uwanda wa juu wa Shule ya Msingi Gendabi.
“Nilikiona kifo kabisa, lakini ukuu wa Mungu unabaki kuwa ukuu wake. Hayo maporomoko yalipita nyuma ya nyumba yangu nikiyaona nikiwa na wanangu, lakini huwezi amini nilipata ujasiri wa kuwaongoza kukimbilia eneo la milimani na wakati huo sikukumbuka mifugo yangu, hasa ng’ombe.
Neema anasema kuwa baada ya maji kupungua alirudi nyumbani kwake na hakukuta chochote ikiwamo mifugo hiyo ambayo alikuwa akifuga.
“Kwa sasa maisha yanaendelea kama kawaida nikiwa na ujauzito wa mtoto wa 12, lakini inapofika majira ya saa 12 za jioni mimi na familia yangu tunarudi katika hifadhi ambayo ipo katika Shule ya Msingi Gendabi katika Halmashauri hiyo ya Hanang.”
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama, uchunguzi wa kijiolojia uliofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) katika tukio hilo hakukuwa na tetemeko la ardhi, wala mlipuko wa volcano katika Mlima Hanang’.
Mhagama alinukuliwa akisema; “Miamba hiyo ilinyonya maji ya mvua na kuporomoka, na hivyo kutengeneza tope kubwa na kipande hicho kilichomeguka kilinyonya maji na kusababisha mgandamizo na sehemu ya mlima, ikashindwa kuhimili mgandamizo huo na hivyo kutengeneza tope lililoanza kuporomoka kwa kasi na kutengeneza njia kufuata mkondo wa Mto Jorodom.”
Maeneo yaliyoathirika zaidi na maafa hayo ni Mji Mdogo wa Katesh na kata zake, ambazo ni Jorodom na vitongoji vyake vya Udameseki, Gawal na Jorodomu Kati.
Pia zimo Kata ya Gadang’a na vitongoji vyake vya Gadang’a A, Gadang’a B, lakini Kata ya Katesh A na Gedang’ongyi na Kata ya Katesh, vitongoji vya Kates Stendi na Katesh B.
Aidha, zimo pia Kata ya Gendabi, Kijiji cha Gendabi katika vitongoji vya Uhuru na Dumanang’.
Mmiliki wa nyumba ya kulala wageni Gendabi, Samson Israel, alimwomba Rais, Samia Suluhu Hassan, kuona uwezekano wa kuwahamisha katika eneo hilo, kwa kuwa kwa sasa halifai kuishi binadamu.
MISAADA YAMIMINIKA
Jana Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, alieleza kuwa serikali imeendelea kupokea na kugawa misaada ya chakula na mahitaji muhimu kwa waathirika wa maafa ya Hanang’ mkoani Manyara.
Alisema hadi kufikia jana misaada ya chakula na mahitaji muhimu imefikia thamani ya Sh. bilioni 2.5 na fedha taslimu Sh.bilioni 5.2.
Alisema fedha taslimu zinajumuisha shilingi bilioni 2.5 zilizoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Sh.bilioni 2.7 zilizomo kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 2.2 zimechangwa na taasisi na mashirika ya umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na Sh. milioni 419.4 zimechangwa na wahisani mbalimbali.
Matinyi alisema: “Wakati serikali ikiwashukuru Watanzania kwa utu, upendo, uzalendo na moyo wa kujitolea ambao umesaidia kupatikana kwa chakula cha kutosha na mahitaji muhimu ili kuwasaidia waathirika kuendelea na maisha yao, inatoa wito pia kwa wanaoendelea kuleta misaada kujikita zaidi katika vifaa vya ujenzi.”










