Mandonga anatarajia kupigana na Mti Jitu katika pambano lililopangwa kufanyika Desemba 29, mwaka huu mkoani, Morogoro.
Akizungumza na Nipashe, Mandonga alisema kwa sasa ameamua kuja tofauti na kwa kutumia jina hilo la Chifu Kingalu Mwanabanzi, anaamini atampiga ngumi sehemu yoyote mpinzani wake.
"Bondia Mti Jitu atakutana na ngumi inayoitwa Chifu Kingalu Mwanabanzi, hiyo ngumi imebarikiwa, hiyo ngumi ukitaka mvua inakuja tukiomba jua linakuja, kwa hiyo akae akijua kama Jiti Mawe siku hiyo tutambatiza na kumwita Mama Jiti Mawe, maana atachakazwa na ngumi hiyo” alisema Mandonga.
Naye Mti Jitu alisema hatishwi na vituko vya Mandonga kwa sababu ngumi zake hazimtii hofu na yeye tayari ametumia nguvu ya milima ya Ng’aro, Chamanyani na Mizimu ya Kolelo ili kuibuka na ushindi.
Katibu wa Chama cha Ngumi Mkoa wa Morogoro, Hassan Athuman (Banda), alisema chama hicho kinaendelea kujipanga kuendeleza mabondia vijana ili wapate mafanikio na si kutoa burudani pekee.
Banda alisema wanatarajia kuweka mazingira bora ya kutoa ajira kwa mabondia kupitia ngumi kama ilivyo katika michezo mingine.
Mkurugenzi wa Kimbeho Talents Promotion, waandaaji wa pambano hilo, Majaliwa Kimbeho, ametoa wito kwa wakazi wa Morogoro kujitokea kushuhudia mabondia hao wakipambana lakini pia kupata burudani ya kufunga mwaka.
Kimbeho alisema busara imewaongoza kuwahamasisha vijana wa Morogoro kushiriki katika mchezo huo kutokana na historia ya kufanya vizuri katika tasnia mbalimbali ikiwamo muziki na soka.










