Pia amewataka kulisaudia jeshi hilo katika utatuzi wa migogoro ya ardhi, mauaji ya kujichukulia sheria mkononi, wizi pamoja na unyang'anyi wa kutumia silaha.
SACP Mutafungwa ametoa kauli hiyo Desemba 21, 2023 kwenye mkutano wake na waganga hao zaidi ya 500 katika ukumbi wa kihistoria wa Mahatma Gandhi mkoani hapa.
Amewataka wataalamu hao kuwa sehemu ya kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka ili kuhakikisha wanapunguza matukio ya mauaji na uharifu.
"Tunatamani kuona uharifu unaisha katika Mkoa wa Mwanza ili ifike hatua matukio ambayo yanakuwa yakileta hofu katika jamii yetu yanaisha mfano mauaji ya kutokana na imani potofu za kishirikina, migogoro ya ardhi, matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto, kuwania mali, unyanganyi, wizi, pamoja na utapeli na ndio maana tumewaita leo ili kuzungumza na kuona namna gani mnaweza kusaidia katika kupunguza vitendo hivyo kwa sababu nyie ni kundi muhimu," amesema SACP Mutafungwa.
Mkuu wa Upelele wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Mratibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Yesaya Sudi amewaasa waganga wa tiba asilia kuwafichua wapiga ramli chonganishi katika jamii kwani wao ndio wamekuwa chanzo cha kuchafua sifa ya taaluma hiyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asilia mkoa wa Mwanza, Shabani Ramadhani akizungumza kwa niaba ya kundi hilo ametoa wito kwa waganga wenzake kutoa taarifa ya waganga wale wasiofuata sheria huku akimpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Hospitali za Rufaa kuwa na kitengo cha tiba asilia.
Kuhusu hali ya ulinzi na usalama mkoani Mwanza, kamanda Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi lipo imara na limejipanga vizuri kuhakikisha linawasimamia na kuwaelekeza wananchi na ikiwezekana kuchukua hatua za kisheria kwa watakao fanya uhalifu kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka 2023.










