Umoja wa Makanisa ya CPCT yafariji waathirika wa maafa Hanang

10Dec 2023
Na Mwandishi Wetu
Manyara
Nipashe Jumapili
Umoja wa Makanisa ya CPCT yafariji waathirika wa maafa Hanang

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama ameishukuru uongozi wa umoja wa Makanisa ya Kipentencoste Tanzania (CPTC)..

Umoja wa Makanisa ya CPCT watoa mifuko 500 ya saruji kama sehemu ya msaada wa kibinadamu kuwafariji wa waathirika wa maporomoko ya Mawe na Matope kutoka Mlima Hanang, Mkoani Manyara.

..kwa namna walivyoendelea kuonesha upendo kwa kuchangia mifuko 500 ya saruji kwa waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope na mawe kutoka Mlima Hanang’ mkoani Manyara na kuendelea kuwaombea waathirika hao.

 

Ameyasema hayo mapema Desemba 9, 2023 katika ibada iliyoandaliwa na umoja wa makanisa hayo iliyofanyika katika kanisa la DNPC-Katesh.

 

Waziri Mhagama alishukuru namna kanisa linavyoendelea kusaidia jamii katika malezi ikiwemo kuwalea kiroho na kusema hii inasaidia Serikali kuwa na vijana na Taifa lenye maadili mema.

 

“Kanisa ni taasisi muhimu sana, endeleeni kutushauri pale inapobidi na ninawashukuru namna mmeendelea kuungana nasi katika maafa haya kwa kutoa mifuko ya Saruji nasi tutaiwasilisha niwahakikishie itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa usimamizi mzuri wa Serikali yetu,” alisema  Mhagama

 

Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentencoste Tanzania (CPTC) Dk. Barnabas Mtokambali ameshauri jamii kuendelea kuwaombea waathirika wa maafa hayo huku akitoa rai kuona umuhimu wa kuwapa msaada kwa namna yoyote ili kusaidia na kuonesha upendo kwa matendo lengo ni kuendelea kushikamana kama watanzania.

 

“Ni wakati sahihi kuwakimbilia ndugu zetu hawa, tuwaoneshe upendo na Serikali imechukua jukumu hili nasi tuungane nao kwa kuwasaidia ndugu zetu na tukumbuke bado serikali inawahudumia hata wakiwa katika makazi yetu,” alisema Mchungaji Mtokambali.

 

Ametahadharisha uwepo wa changamoto kadhaa zinazoweza kusababishwa na mikusanyiko ikiwemo magonjwa ya milipuko, mmomonyoko wa maadili na tabia zingine zisizofaa na kuwaomba waumini na jamii kwa ujumla kuendelea kuwaombea na kuwastiri kwa namna mbalimbali.

 

Naye Mbunge wa Hanang Mhandisi Samwel Hayuma alieleza kuwa amefarijika kwa namna kanisa lilivyowakimbilia na kuendelea kuwaombea katika mapito ya maafa yaliyotokea Wilayani Hanang.

 

Aidha alimshuku Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kujali na kutoa maelekezo kwa viongozi wake kuratibu na kuhakikisha hali inarejea katika nafasi yake.”

 

“Mhe Waziri mhagama wewe ni mpambanaji kweli, umefanya kazi kubwa katika kuratibu maafa haya, hakika Serikali inafanya kazi nzuri sana na hii imetupa faraja kubwa kuona Serikali yote ipo hapa Hanang’ tunasema asanteni sana,” alisisitiza Mhandisi Hayuma

 

Aidha alitumia nafasi hiyo kuwaasa Watanzania kuungana Pamoja kuendelea kumuombea mbeba maono wa nchi hii ambaye ni  Rais kwa namna anavyotuongoza Pamoja na wasaidizi wake wote.

 

“Tuone umuhimu na haja ya kuendelea kumuombea sana Rais wetu na viongozi wote wa nchi yetu, Tanzania ni nchi nzuri yenye upendo wa hali ya juu, Tuendelee kuiombea Hanang’ yetu, Manyara yetu na Nchi kwa ujumla,” alisema