Benki ya Ushirika Kilimanjaro yang'ara tuzo za NBAA

04Dec 2023
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Benki ya Ushirika Kilimanjaro yang'ara tuzo za NBAA

BENKI ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL), imepata tuzo ya umahiri baada ya kuibuka ya kwanza katika uandaaji mzuri wa hesabu kwa sekta ya kifedha na kibenki katika makundi ya Taasisi za Fedha nchini.

Meneja Mkuu wa Benki ya Kilimanjaro(KCBL), Godfrey Ng'urah.

Tuzo hiyo ilitolewa na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) katika hafla iliyofanyika Bunju Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja Mkuu wa Benki hiyo, Godfrey Ng'urah, alisema ushindi huo umewapa faraja kubwa baada ya kupitia changamoto ya kimtaji kwa miaka mingi.

"Kwa kweli tumetuma ujumbe kwamba Ushirika unaweza. Na hakuna aliyeamini kwamba tungepata ushindi huu na kuwa miongoni mwa benki bora inayoweza kuandaa hesabu zake vizuri baada ya kupitia changamoto ya kimtaji,"alisema Ng'urah.

"Nitoe shukrani kwa Bodi na kwa Wanahisa ambao wameendelea kutuamini pamoja na kuwa na historia ambayo siyo chanya sana. Tulipoanza mageuzi haya benki ilikuwa imepata taarifa za mashaka na zisizoridhisha kwa miaka 10 iliyopita lakini ndani ya miaka mitatu tumetengeneza taarifa zilizoibuka kidedea kwa tasnia nzima ya kibenki."

Alisema wanaamini kwamba katika mageuzi wanayoyafanya katika benki hiyo, wako mbioni kuanzisha benki ya Taifa ya Ushirika.

"Hiki ni kiashiria cha msingi bora kutokea kwenye benki hii kwenda kuanzisha benki bora inayozingatia weledi, ubunifu katika kuandaa hesabu zake, utawala bora, kufuata taratibu za sera za ndani ya taasisi lakini miongozo ya Bodi ya Wahasibu nchini na ya Benki Kuu,"alisema Ng'urah.

Alisema wanaamini misingi hiyo itawawezesha kuwa na uhakika kwamba benki ya Taifa ya Ushirika itakayoanzishwa na kumilikiwa na Wanahisa wenyewe, itazingatia misingi ya uandaaji bora wa taarifa za kifedha duniani.

Tuzo hizo za NBAA hutolewa kila mwaka kwa kushindanisha wizara, taasisi, mashirika na kampuni mbalimbali nchini.