Madiwani wawatimua watumishi kwa ulevi

03Dec 2023
Thobias Mwanakatwe
MKALAMA
Nipashe Jumapili
Madiwani wawatimua watumishi kwa ulevi

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, limewafukuza kazi na kuwasimamisha watumishi wanane kwa tuhuma za kushindwa kutekeleza majukumu na ulevi.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, James Mkwega, alikiambia kikao cha baraza hilo wakati wa kujadili utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha wa 2023/24.

Aliwataja watumishi hao kuwa ni mtabibu msaidizi  na muuguzi wa zahanati za halmashauri hiyo.

Makwega alisema watumishi hao wamepewa adhabu hiyo kwa kosa la utoro kazini kwa zaidi ya siku tano bila kutoa taarifa kwa mwajiri.

Aliwataja watumishi wawili waliopewa adhabu ya kukatwa mshahara kwa asilimia 15 kwa miaka mitatu kutokana na ulevi uliokithiri ni ofisa manunuzi msaidizi na mteknolojia mwandamizi wa maabara.

Watumishi wengine waliopewa barua ya onyo kwa kosa la kukiuka taratibu za fedha na manunuzi ni ofisa mtendaji wa kijiji na mteknolojia wa dawa kituo cha afya.

Mwingine ni mtabibu msaidizi ambaye alikuwa akituhumiwa kwa ulevi, baraza limeamuru tuhuma dhidi yake kuchunguzwa upya.

Akizungumza baada ya kusoma maamuzi ya baraza hilo, alisema madiwani hawafurahii kumwita mtumishi kwenye kamati ya uongozi kuhojiwa kwa tuhuma za ulevi.

Aliwataka watumishi kuzitendea haki nafasi zao kwani wapo watu ambao wameenda kwa waganga wa kienyeji na wengine kuombewa ili wapate nafasi za kuteuliwa, lakini hawakufanikiwa.

 

"Mwaka 2014/2015 haikutokea kujadili mtumishi yeyote kwenye kamati ya uongozi, lakini leo hii inatokea mtumishi anajadiliwa kunywa pombe halafu pombe kwanza haijakatazwa kunywa kinachotakiwa usinywe wakati wa kazi," alisema.