Serikali imetangaza mkakati huo, ambao kipaumbele kimewekwa katika kuwapatia ardhi wawekezaji hasa katika sekta ya viwanda ndani ya siku saba tu na kurasimisha makazi ya kaya maskini.
Mageuzi hayo yalitangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akisema mpango huo wa miaka 10 umeanza kutekelezwa kwa kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapimwa na kupangiwa matumizi.
Mradi huo umeanza kutekelezwa mkoani Morogoro na utaendelea nchi nzima huku Lukuvi akisema kuanzia sasa wawekezaji wote nchini ni marufuku kwenda moja kwa moja vijijini kununua ardhi,badala yake wapitie Kituo cha Uwekezaji (TIC) na kama watakwama kupatiwa ardhi waende wizarani.
Tunaipongeza Serikali kubuni na kuanza kutekeleza mkakati huo kwa sababu utasaidia kumaliza ama kupunguza migogoro ya ardhi, ambayo imekuwa sugu karibu maeneo yote nchini.
Migogoro ya ardhi ilishika kasi nchini kuanzia mwaka 2000 ulipoibuka mgogoro mkubwa kati ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro na kusababisha mauaji ya watu.
Migogoro ya wakulima na wafugaji imetokea katika maeneo mengi kwa kutaja baadhi ni Mbarali, Chumya, Korogwe, Kiteto, Mvomero na Rufiji, hivyo kusababisha watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Sababu kubwa ya migogoro hiyo ni Serikali kutopanga matumizi ya ardhi.
Udhaifu huo umekuwa ukisababisha kila kundi kuona lina haki ya kulima au kulisha mifugo katika eneo husika.
Ipo migogoro mingi pia ambayo imekuwa ikisababishwa na wawekezaji kwenda vijijini moja kwa moja kuchukua ardhi bila kupitia TIC au wizarani.
Ingawa sheria ya Ardhi ya Kijiji ya mwaka 1999 inaelekeza kwamba Mkutano Mkuu wa Kijiji una mamlaka ya kumilikisha ardhi kwa mtu yeyote, lakini uzoefu unaonyesha kuwa fursa hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya.
Baadhi ya watu wenye fedha wamekuwa wakitumia fedha zao kuwashawishi na kuwarubuni baadhi ya viongozi na wanavijiji kuwamilikisha ardhi, lakini baadaye inaibuka migogoro mikubwa. Chanzo cha migogoro hiyo ni waliochukua ardhi kubwa kutoiendeleza kwa muda mrefu.
Bila shaka Serikali imejiandaa vya kutosha hususani kibajeti katika kutekeleza na kuufanikisha mpango huo, na ni matumaini yetu kwamba ndani ya miaka 10 migogoro ya ardhi itakuwa imepungua kwa kiasi kikubwa au kumalizika kabisa.
Huko nyuma Serikali imekuwa ikiahidi kwamba itapima ardhi yote nchini, lakini hadi sasa ahadi hiyo haijaonekana kutekelezwa. Hata hivyo, kasi ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano inatoa matumaini kuwa ahadi hiyo itatekelezwa na kwa wakati mwafaka.
Tunasema hivyo kutokana na kuanza kufuta hati za mashamba ambayo hayakuendelezwa muda mrefu kwa ajili ya kuwagawia wananchi.
Mkakati huo umekuja wakati mwafaka kwa kuwa katika siku za usoni ardhi itakuwa na thamani kubwa kutokana na mahitaji kuongezeka hususani wawekezaji watakaokuwa wakizalisha malighafi kwa ajili ya viwanda.
Tunawashauri wananchi kuunga mkono mpango huo kwa kuwa utawanufaisha kwa kuwa ardhi yao itakuwa na thamani baada ya kupimwa.
Kwa upande wake, Serikali ihakikishe inatumia sheria kusimamia utoaji wa ardhi kwa wawekezaji kutoka nje. Kwamba wapitie TIC, lakini wakikwama waende wizarani.
Tunawakumbusha wakuu wa wilaya na mikoa kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha wanasimamia matumizi ya ardhi baada ya kupimwa na kupangiwa matumizi.










