TANROADS kushirikisha serikali za mitaa katika miradi ya ujenzi

22Nov 2023
Hamida Kamchalla
HANDENI
Nipashe
TANROADS kushirikisha serikali za mitaa katika miradi ya ujenzi

WAKALA wa Barabara nchini (TANROADS) wametakiwa kuzishirikisha Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili iwasaidie katika kusimamia miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja mikoani badala ya kutumia mfumo mmoja wa kufanya kazi yenyewe.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ametoa wito huo leo katika kijiji cha Kwamsisi wilayani Handeni alipopita kukagua barabara inayotokea Mkata kwenda wilayani Pangani ambapo wananchi wanalalamika kucheleweshwa kwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ya kiwango cha lami.

Bashungwa amesema, "mfumo wa serikali hata katika vyombo vyake vya usalama kupitia wakuu wa mikoa na wilaya kwa kushirikiana na timu zao katika maeneo yao zipo taarifa nyingine ambazo ziko nje ya utaratibu wa kawaida wa mfumo wako".

"Sasa mifumo yote miwili ikitumika tutaongeza tija ya usimamizi wa hawa wakandarasi na itapunguza swala la ucheleweshaji, kwamba mpaka Waziri afike, tutakwama kwasababu kasi ya kujenga nchi hii chini ya Dk. Samia Suluhu Hassan ni kubwa mno fedha nyingi zinakuja kwa ajili ya kuwatumikia watanzania, kwahiyo mkurugenzi mkuu nenda kajipange vizuri na nione tija ya mipango yako"

Hata hivyo, Waziri amemtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga Eliazary Rweikiza kufanya namna ya kuharakisha wanatekeleza barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe kwanza kabla lami haijawekwa ili wananchi wapate kuendesha shuhuli zao kujiinhizia kipato.