Akizungumza mbele ya wanahabari wakati wa utoaji wa mfano wa hundi kwa washindi wa promosheni hiyo iliyohitimishwa leo, Mkuu wa Kitengo na Usambazaji wa Tigo Pesa, Innocent Mosha, amesema promosheni hiyo ilianzishwa ili kuwapa motisha mawakala katika kutekeleza majukumu yao na pia kuwashukuru kwa kujitoa kikamilifu kupambania malengo ya kibiashara waliyokubaliana kwa pamoja.
Mosha amesema kuwa promosheni hiyo iliendeshwa kwa mwezi mmoja wa Oktoba. "Leo tunawatunuku wale walioweza kufikia malengo yao ya biashara kwa kuwahudumia wateja wetu katika maeneo yao kwa ufanisi mkubwa," amesema na kuongeza kuwa;
"Hii ni siku ya kipekee tunayoweza kusherehekea mafanikio ya mawakala wa Tigo Pesa kutoka maeneo mbalimbali, kama vile Mwanza, Zanzibar, Dar es Salaam, Arusha na Mbeya,ambapo kwa ujumla mpaka leo tutakuwa tumetoa zaidi ya sh. milioni 300 kwa mawakala walioibuka washindi," amesema.
Ameongeza kuwa unapozungumzia juu ya mafanikio hayo, ni muhimu kutambua wigo mpana wa huduma za Tigo Pesa.
Kwa mujibu wa Mosha Tigo Pesa inatoa huduma kamili za kifedha kwa zaidi ya wateja milioni 13 na ili kutoa huduma kwa ufanisi, lazima tuwawezesha mawakala ambao ni washirika wao muhimu wa biashara ambao kupitia Tigo Pesa Wakala wanachangia kiasi kikubwa kufikisha huduma za kifedha kwa watanzania wote.
"Tigo Pesa inajivunia wafanyabiashara 300,000 wanaotoa huduma za Lipa kwa Simu na takriban wakala wa Tigo Pesa 200,000 nchi nzima, vile vile Tigo Pesa tunaendelea kuwaletea wateja huduma za kibunifu zinazochangia ukuaji uchumi wa kidigitali hapa Tanzania kama vile Bustisha, Tigo Pesa Rafiki, Kibubu, Nivushe Plus, Tigo Kilimo, Bima Mkononi, na nyingine nyingi," amesema.










