Wadau wakutana kujadili changamoto zinazowakabili walemavu

15Nov 2023
Pilly Kigome
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau wakutana kujadili changamoto zinazowakabili walemavu

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), wamekutana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuandaa ripoti yenye lengo la kufahamu changamoto zinazowakabili walemavu nchini.

Hiyo imekuja kwa kuelekea kwenye maadhimisho ya siku ya walemavu Zanzibar yatakayofanyika Desemba mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mratibu Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema kumekuwa na changamoto nyingi zinazowakabili watetezi wa walemavu na kupelekea kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Hivyo ripoti hiyo itaandaliwa na makundi yanayofikia 14 ya makundi mbalimbali ikiwemo wanaotetea haki za watoto, wanawake, wakimbizi, walemavu na hata mifugo kuandaa ripoti za utafiti ambazo zitasidia kujua njia za kutatua.

Amesema ripoti hiyo itasaidia kujua ni changamoto gani zaidi zinazowakabili walemavu kwani wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi zaidi na wamekuwa hawawezi kusimama wenyewe.

“Tumeona tuangalie kile kinachosumbua taasisi ili kupata nafuu ya kuweza kuwasaidia wanaowatetea walemavu, maana kama wanaowatetea walemavu wanachangamoto vipi kwa walemavu wenyewe" amesema Olengurumwa.

Amesema walemavu wanakabiliwa na mazingira magumu hasa mikoani na pembezoni mwa mji changamoto nyingi zinazowakabili ikiwemo masuala ya afya,elimu, uchumi na hata siasa ambapo wamekuwa wakilalamika kutengwa katika jamii na kukosa haki stahiki.

Olengurumwa amesema kuna sheria ambazo zimewekwa na Serikali lakini hazifuatwi na kusababisha ugumu wa kazi kwa watu wenye ulemavu hivyo wanaona kunahaja ya kufanyia marekebisho ili zifuatiliwe.

Pia amesema ukata wa fedha kwa taasisi za walemavu ni chanzo cha kutofanyika kazi zinazokusudiwa licha ya kuwepo kwa wafadhili ambao wanatoa fedha lakini haziwafikii walengwa.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu,kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu,Joy Maongezi, amesema ripoti ya utafiti ya tathimini ya watu wenye ulemavu wataitumia kwa ajili ya kupitia sera,sheria na miongozo ya kutathimini uhitaji wa watu wenye ulemavu kwani ofisi hiyo ndiyo yenye dhamana na watu wenye ulemavu.

Maongezi amesema Serikali imekuwa ikipingana na tabia ya watu kuwatumia walemavu kujipatia kipato,hivyo kuna haja ya kuandaa sheria itakayosaidia kukabiliana na mambo hayo ikiwemo na kuondolewa sheria za zamani.

Naye Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Taifa la watu wenye Ulemavu Zanzibar Husi Khamis Dede amesema ripoti hiyo jumuishi itakayotolewa itasaidia Serikali kuona changamoto na kuweza kuzifanyia kazi.

Amesema Zanzibar kukabiliana na watu wenye ulemavu tayari kuna sheria mpya zimeundwa mwishoni mwa mwaka 2022, kuna Baraza la walemavu lipo chini ya Serikali.

Vilevile amesema kuna mfuko wa maendeleo wa watu wenye ulemavu umeanzishwa,ikiwemo na kuanzishwa mabalaza ya watu wenye ulemavu.

Amesema tayari kutokana na umuhimu wa watu wenye ulemavu Serikali ya Zanzibar wameshatengeneza shule mbili za watu wenye ulemavu ambazo zimeingia kwenye historia tangu kupatikana kwa uhuru.

Kwa upande wake Ernest Kimaya Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu Tanzania amesema nafasi waliyopewa kupitia utafiti uliyofanywa itawasaidia kuboreshwa kwa haki za watu wenye ulemavu ikiwepo Sera, Sheria na miongozo.

"Imebainika tafiti za awali zimeona sisi watu wenye ulemavu tuko katika kipindi kigumu hivyo sera hzi mpya zinakwenda kuona umuhimu wetu katika Taifa," amesema.