-huku akiweka wazi haitakuwa mechi rahisi.
Michuano hiyo inayoshirikisha Klabu nane bora zaidi barani Afrika, ambazo ni Al Ahly (Misri), Wydad Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Esperance Tunis (Tunisia), Simba (Tanzania), Petro Atletico de Luanda (Angola), Enyimba FC (Nigeria) na TP Mazembe (DR Congo), itaanza Ijumaa wiki hii kwa mechi ya ufunguzi kupigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Pia michuano hiyo itachezwa kwa mtindo wa mtoano nyumbani na ugenini ambapo baada ya mechi hiyo ya Ijumaa, Simba itashuka tena dimbani ugenini dhidi ya Al Ahly Jumanne ya wiki ijayo nchini Misri na mshindi wa jumla atatinga nusu fainali.
Akiuzungumzia mchezo huo, Robertinho alisema anafahamu itakuwa ngumu kwa sababu Al Ahly ina uzoefu wa mechi nyingi za kimataifa na kwa aina ya uchezaji wao anatengeneza mfumo wa kukabiliana nao.
"Natakiwa kuwa makini kutengeneza mfumo kwenye eneo la katikati, viungo wakabaji na viungo washambuliaji ndiyo hapo tunaweza kukabiliana nao, ila naamini tutafanya vizuri kutokana na mwenendo tunaokwenda nao kwenye Ligi Kuu na tulioonesha katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Mashabiki wawe na imani kwa sababu timu inaendelea kutengenezwa na tayari kila mtu anaona imeshaanza kuimarika," alisema Robertinho.
Katika eneo la safu ya kiungo ya ukabaji ya Simba ambayo Robertinho amesema anatengeneza mfumo sahihi wa kuweza kuithibiti Al Ahly, kawaida imekuwa ikiongozwa na Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute huku kiungo cha ushambuliaji mara nyingi kikiwa chini ya Clatous Chama, Kibu Denis na Saido Ntibazonkiza.
Kuhusu maendeleo ya golikipa Aishi Manula ambaye Jumamosi iliyopita Robertinho alimpa dakika 40 wakati wakishinda mabao 5-1 kwenye mechi ya kirafiki ya kimazoezi dhidi ya Dar City FC iliyopigwa Uwanja wa Mo Arena, alisema pamoja na kutaka kuwapa utimamu wa mwili wachezaji wake wote na kuangalia mapungufu, lakini ilikuwa ni kumwangalia kipa huyo kama atakuwa yupo tayari kukaa langoni.
Kipa huyo ambaye aliumia Aprili 7 mwaka huu katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Ihefu, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Simba ikishinda mabao 5-1, katika mchezo huo dhidi ya Dar City alionekana kuwa fiti.
Robertinho alisema Manula alionesha kuwa fiti kwa dakika 40 alizocheza kabla ya kumpisha kipa mwingine aliyesajiliwa kutoka KMC, Hussein Abel.
"Amekaa langoni lengo ilikuwa ni kumwangalia kama atakuwa yuko fiti, nimemwona na anaweza kukaa langoni Ijumaa, lakini hiyo pia itategemea pia ushauri wa pamoja kutoka kwenye benchi la ufundi pamoja na madaktari," alisema.
Alisema pamoja na yote, maendeleo ya kipa huyo yanampa uhakika wa kuwa na nguvu mpya kwenye eneo la langoni na hasa katika mechi ya marudiano nchini Misri, kwani hata kama ikitokea hakucheza Dar, inawezekana kabisa akawa langoni mechi ya marudiano.
Robertinho alisema mchezaji mwingine aliyekuwa majeruhi Henock Inonga kwa sasa hana tatizo lolote na moja kwa moja atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoivaa Al Ahly.
Inonga ambaye aliumia Septemba 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, alipokanyagwa na mchezaji wa Coastal Union, Haji Ugando kwa sasa yupo na kikosi cha Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kwa mujibu wa Robertinho amepona na hana tatizo lolote.










