Mnyika aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha mafunzo cha Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) kilichokuwa kikijadili mada mbalimbali.
Mnyika alisema katiba inapaswa kurekebishwa na sheria zote ziendane na marekebisho hayo ili nchi inapoingia kwenye uchaguzi kuanzia wa serikali za mitaa mwakani, kuruhusu Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) isimamie.
“Nitoe wito kwa serikali kwa Rais na wadau wa demokrasia kinachotakiwa kufanyika katika taifa letu kwa sasa kwa haraka ni mambo matatu. Moja, kupelekwa bungeni muswada wa sheria wa kuendeleza mchakato wa katiba ili tuianze safari ya kupata katiba mpya katika taifa letu,” alisisitiza.
Mnyika alitaja jambo la pili ni kupeleka bungeni muswada wa sheria ya marekebisho ya katiba ya mwaka 1977, ili safari ya katiba mpya kutokana na kucheleweshwa kwa watawala wanapokwenda kwenye uchaguzi iwe imefanyiwa marekebisho yanayohusu uchaguzi.
Alisema, hiyo itawezesha kuweka mazingira ya kuwa na uchaguzi huru na haki ikiwamo wakurugenzi kuondolewa kusimamia uchaguzi.
Jambo la tatu, alisema ni kupelekwa kwa miswada ya sheria kwa kuwa hawawezi kupeleka miswada inayopingana na katiba, lazima irekebishwe mifumo ya katiba ndipo sheria zitengenezwe.
Mnyika alisema awali kulikuwa na matumaini makubwa kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ataanzisha mchakato wa katiba lakini baada ya miezi michache, matumaini hayo yakavurugwa.
Alisema baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kukamatwa taifa likawa halizungumzi tena mchakato wa katiba na kujikuta wanatumia muda mwingi kukimbizana mahakamani kutafuta haki.
Mnyika alisema Mbowe baada ya kutoka alikutana na Rais Samia wakaanza mazungumzo na kuonyesha matumaini ya kuanza kwa mchakato wa katiba.
“CCM nao walikubali mchakato wa katiba uendelee. Ilikuwa Julai 22, 2022 na tulikuwa na matumaini ya maneno, hapakuwa na matendo. Ikafika Desemba tukawakumbusha mbona tumekwama? ilipofika Januari, mwaka huu, Rais Samia akaondoa zuio la mikutano ya hadhara na kuahidi kuunda kamati ya kuendelea na mchakato wa Katiba mpya.
“Rais alitamka kwamba inabidi wananchi wapewe elimu ya katiba ndiyo mchakato uendelee. Kwa msingi huo, ina maana Rais ametupiga kauli ambayo ilikuwa imetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria kwamba, Watanzania wapatiwe elimu ya katiba kwa miaka mitatu jambo ambalo haliwezi kukubalika,” alisema.
Mnyika aliitaka BAWACHA kujadili kauli hiyo na kuja na tamko lao kuhusiana na suala hilo.
Alisema, Rais alieleza anakusudia kuunda kamati kuhusu mchakato wa katiba na kwamba atavialika vyama kuwasilisha wajumbe, ingawa hakuongea chochote kupeleka bungeni muswada wa sheria utakaoweka utaratibu wa kuendeleza mchakato wa katiba.
“Matatizo mengi yanaanzia kwenye katiba ikiwamo muundo wa tume, katiba inazuia matokeo ya Rais kupingwa mahakamani, inazuia mgombea binafsi, katiba inafanya wanawake wasiwe asilimia 50 kwa 50 bungeni kwa sababu ya muundo wa katiba,” alibainisha.










