Akiuliza maswali bungeni jana, mbunge huyo alihoji kwa nini serikali haifanyi utafiti wa bei za safari za ndege ndani ya nchi kutokana na bei hizo kuwa kubwa.
“Kwa mfano Dodoma hadi Dar es Salaam bei ni kuanzia Sh.250,000 hadi Sh. 500,000 kwa safari ya mara moja. Serikali haioni hatari ya kupoteza soko la ndani endapo yakajitokeza mashirika mengine? Kuna shirika linafanya safari hiyo ya kwenda na kurudi kwa Sh. 450,000. Kwa nini msiokoe ATCL isije kuzama?” alihoji.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, alisema kwa kawaida nauli za safari za ndege hupangwana soko kulingana na aina ya huduma inayotolewa.
“ATCL kama ilivyo kwa mashirika mengine ya ndege yanayotoa huduma zake kibiashara, nauli zake zinapangwa na soko kwa kuzingatia matakwa ya sheria za ushindani. Vigezo vinavyotumika katika kupanga nauli hizo ni pamoja na gharama za uendeshaji ili kuhakikisha mashirika ya ndege yanahimili ushindani wa soko na kujiendesha kwa tija na ufanisi,” alisema.
“Utafiti umekuwa ukifanyika na watafanya zaidi. Kwa sasa ATCL haijapoteza soko na viwango vilivyowekwa ni kwa mujibu wa ushindani,”alisema.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo, alihoji mpango wa serikali wa kuhakikisha zinapatikana ndege za moja kwa moja za Dodoma kwenda Kilimanjaro na Arusha au muda mfupi wa kuunganisha kupitia Dar es salaam.
Akijibu swali hilo, Kihenzile alisema serikali imepokea ushauri huo na itafanyia kazi.









