Ajali ya basi, Coaster na Lori yajeruhi wanne Mbeya

16Jul 2023
Na Mwandishi Wetu
Mbeya
Nipashe Jumapili
Ajali ya basi, Coaster na Lori yajeruhi wanne Mbeya

WATU wanne wamejeruhiwa katika ajali iliyotokea wilayani Mbarali, mkoani Mbeya baada ya Coaster kugongana na basi la kampuni ya Fikosh linalofanya safari kutoka Mwanza Kwenda Mbeya.

Akizungumza na chombo kimoja cha Habari, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Mstaafu Denis Mwila amesema ajali hiyo imetokea saa 12.30 alfajiri katika kona iliyopo Kata ya Igurusi, Tarafa ya Ilongo.“Ni kweli ajali hiyo imetokea leo ambapo basi la Kampuni ya Fikosh lililokuwa linatokea Mwanza kuja Mbeya limeigonga costa inayofanya safari kutoka Ubaruku kuja Mbeya na kusababisha kugongana na uso kwa uso na gari lingine (Lori) kisha kuanguka pembezoni mwa barabara,”amesema.Ameongeza kuwa Coaster iliyogongwa kwa nyuma ni mali ya Umoja wa Madereva Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva Hemedy Bamboya (46).Aidha, Kanali Mstaafu Mwila amewataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Mathias Mashala (59) Mkazi wa Wilaya ya Mbozi, Justina Stephano (Mkazi wa Mbozi), Ngimba Mashala (43) na Ombeni Given (23) wote walikuwa wakisafiri kwenye basi la Kampuni ya Fikosh lililokuwa likitokea Mwanza kuja Mbeya.