Julai 18, mwaka huu, Rais Magufuli aliagiza kuwa vikosi vya ulinzi na usalama, likiwamo Jeshi la Polisi, vinapaswa kusafishwa kwa kuwaondoa watumishi ambao si waaminifu, ambao wanadai kuleta taswira mbaya ndani ya taasisi hizo, zikiwamo tuhuma za ubadhirifu.
Kutokana na kuwapo kwa tuhuma hizo, Rais Magufuli aliagiza kuwa ni vyema sasa kazi zote zikiwamo za kitaalamu kama uhasibu, utawala na uhandisi zikafanywa na askari ambao wamesomea fani husika. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kudaiwa kuwa baadhi ya watumishi ambao si askari kuwa wakijihusisha na ubadhirifu hivyo kuharibu taswira ya jeshi hilo.
Katika kutekeleza agizo hilo, ndani ya Jeshi la Polisi pekee, watumishi 600 ambao si askari wameshaondolewa na kupelekwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ambako watangangiwa majukumu mengine.
Mbali na polisi, taarifa zaidi zinaeleza kuwa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zaidi ya watumishi raia 100 wameondolewa na kwamba watapangiwa kazi zingine katika utumishi wa umma.
Ni ukweli kwamba hatua hiyo itawezesha kusafisha taasisi hizo na kurejea katika taswira yake halisi ambayo ilitoweka miaka kadhaa, kutokana na sababu mbalimbali kama vile ubadhirifu, lakini pia itatoa nafasi kwa askari kusomea fani mbalimbali na kuwa na wataalamu wengi waliobobea katika taaluma anuai ndani ya majeshi.
Uamuzi huo utatoa pia nafasi ya kuwapo kwa maadili ya kiwango cha juu, ikiwamo utunzaji siri ndani ya taasisi hizo zenye dhamana ya ulinzi na usalama wa taifa.
Hata pale panapotokea mmomonyoko wa maadili miongoni mwa askari, itakuwa rahisi wahusika kuchukuliwa hatua stahili, tofauti na sasa kwa kuwa mtu ambaye si askari akifanya kosa, hatachukuliwa hatua za kijeshi bali zile za utumishi wa umma ambazo huchukua mlolongo mrefu na hata muda pia.
Pamoja na kwamba uamuzi wa kuwaondoa raia katika utumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama nchini ni mzuri, suala la nidhamu na maadili ndani ya vyombo hivyo, hususan polisi, linapaswa kuangaliwa kwa mapana zaidi. Tunasema hivyo kwa sababu kwa kiasi kikubwa taswira ya Jeshi la Polisi, imeharibiwa kwa kiasi kikubwa na askari wenyewe.
Baadhi ya askari wasio waaminifu wameshiriki kuharibu sifa ya jeshi hilo kutokana na kutuhumiwa kushiriki katika matukio ya ujambazi, mauaji ya raia, kubambikia kesi raia, rushwa na vitendo vingine vinavyokwenda kinyume cha maadili ya jeshi hilo. Wanaoongoza magari barabarani, wanaoendesha doria na ulinzi katika benki kwa sehemu kubwa ni polisi na miongoni mwao wamedaiwa husika katika vitendo viovu ambavyo vinakiuka maadili.
Kwa mantiki hiyo, bado kazi kubwa inahitajika kuhakikisha Jeshi la Polisi na vikosi vingine vya ulinzi na usalama vinarejeshwa katika weledi unaotakiwa na hatimaye wananchi kuwa na imani navyo.
Baada ya watumishi ambao si askari kuondolewa katika vikosi hivyo, ni imani kwamba kutakuwa na nidhamu katika utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu mbalimbali utakaofanyika katika mfumo wa kijeshi zaidi.
Hata hivyo, ni wajibu wa viongozi wakuu wa jeshi hilo pamoja na wale waliopewa dhamana ya kuongoza maeneo mbalimbali kama vile usalama barabarani, kutuliza ghasia, kufanya doria na upepelezi kuhakikisha watendaji walio chini yao wanafanya mambo kwa kufuata taratibu na sheria.
Iwapo hayo hayatatekelezwa kwa vitendo, ni dhahiri kwamba imani hasi waliyo nayo baadhi ya wananchi kuhusu polisi na baadhi ya vikosi vya ulinzi na usalama itaendelea kuongezeka.
Kinachotakiwa baada ya utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli, ni vikosi vya ulinzi na usalama, kuhakikisha vinajipanga upya katika kutekeleza dhana halisi juu ya usalama wa raia na mali zao na hatimaye kurejesha imani yake kwa wananchi.










