Mwenge wazindua jengo la dharura Hospitali ya Mkoa

23Apr 2023
Gideon Mwakanosya
SONGEA
Nipashe Jumapili
Mwenge wazindua jengo la dharura Hospitali ya Mkoa

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023, Abdallah Shaibu Kaimu, ameridhia kuzindua jengo la dharura la Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma, lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh. milioni 630.

Kaimu alisema ameridhia kufungua jengo la kutolea Huduma za Dharura (EMD) hospitalini hapo ambalo limekamilika kwa asilimia 100.

Aliwataka madaktali, wauguzi pamoja na watumishi wengine kuyatunza mazingira yote ya miundombinu ya majengo ya hospitali hiyo likiwamo jengo la dharura lililojengwa kwa gharama kubwa.

Pia aliwataka wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi kwa kutoa huduma bora kwa wateja wao.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Magafu Majura, alisema hospitali hiyo ni miongoni mwa 28 za rufani nchini, ikipandishwa hadhi mwaka 1964 na ina watumishi 431 wa kada mbalimbali.

Dk. Majura alisema baada ya kuwapo ongezeko kubwa la wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali hiyo hasa wa dharura, uongozi hospitalini hapo ulianza mchakato wa kuiomba Wizara ya Afya kujengewa jengo lenye nafasi kubwa ya kutoa huduma hiyo.