Kwa kuzingatia hilo, Zitto amesema hawatoacha kusema wanapoona maslahi ya wananchi yanakanyagwa.
Alitoa kauli hiyo jana kwenye mkutano wa chama uliofanyika kisiwani Pemba kwenye Uwanja wa Tibirinzi ambako pia waliwapokea wanachama wapya 305 kutoka Chama cha Wananchi (CUF), 10 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mmoja toka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Zitto alisema kwamba chama, licha ya alichokiita madhila yaliyotokea mwaka 2020, waliamua kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kujenga serikali inayowajibika kwa watu.
"Hatukuingia kwenye serikali ili kujenga serikali ambayo haiheshimu sheria za nchi, serikali ya namna hiyo sio serikali ambayo tunaweza kuendelea nayo. Tunataka serikali inayowajibika kwa watu.
"Na sisi kama chama ambacho tumo ndani ya serikali hiyo, ni lazima tuhakikishe uwajibikaji. Tunapoibua masuala ya watu, maslahi yetu ni watu. Bahati mbaya sana baadhi ya viongozi kwa kuwa wao uongozi ni maslahi yao, wanadhani kila mtu mwingine uongozi unaangalia maslahi yake.
"Sio sisi ACT-Wazalendo. Sisi uongozi ni maslahi ya watu, mtu ambaye anaweza akathubutu kwenda kusema kwamba 'hao ACT wanaibua hili na hili, watangaze kwanza maslahi yao', tunatangaza maslahi yetu ni Wazanzibar, hatutoacha kusema tunapoona maslahi yanakanyagwa," alisisitiza.
Alisema wataendelea kuwasemea wananchi mpaka wapate Zanzibar mpya, Zanzibar moja na yenye mamlaka kamili.
Zitto pia alikumbusha maneno ambayo Maalim Seif Shariff Hamad (hayati) aliwahi kuyasema kwenye uwanja huo mwezi Desemba mwaka 1987, kwamba "Nipo nanyi sasa hivi, ninawaahidi nitakuwa nanyi nikiwa ndani ya serikali au nje ya serikali, ninawaahidi nitakuwa nanyi nikiwa ndani ya chama au nje ya chama."
Zitto alisema jambo la msingi Maalim aliwaahidi Wazanzibar kwamba atakuwa nao ndani ya chama au nje ya chama, wakati ambao kulikuwa hakuna chama kingine.
"Maalim aliona huko mbele lazima kuwe na mageuzi, yakatokea na vyama vikatokea, akatuachia wajibu huu ambao tunapaswa kuutekeleza. Na mimi ninawaahidi wananchi wa Pemba, Wazanzibar tutakuwa nanyi wakati wote.
"Tuwe ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa au nje ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, tupigwe mabomu au tusipigwe mabomu, tutekwe au tusitekwe, tuumizwe au tusiumizwe, tutakuwa nanyi mpaka pale tutakapohakikisha haki zinaheshimiwa na Zanzibar yenye mamlaka kamili inafikiwa," alisema.
Zitto alifafanua kuwa ameona aseme maneno hayo kwa kuwa wanao wajibu wa kukumbushana.
Alisema hawako kwenye siasa kwa sababu wanapenda kuwa huko, bali kwa sababu kuna masuala ambayo wanayapigania, ikiwa ni pamoja na haki za watu, uwajibikaji na demokrasia.
Alisema hiyo ndio sababu wanapigania mchakato wa Katiba Mpya ili waipate itakayojali haki za watu, uongozi unaowajibika kwa watu na itakayojenga mwafaka wa kitaifa.
Alisema wanaitaka serikali kwa haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa mapendekezo yaliyotolewa kwenye taarifa ya kikosi kazi, taratibu na mchakato wa Katiba Mpya uanze mara moja.
Pia alisema suala la sheria ya uchaguzi ili kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kupitia sheria mpya ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa ni mambo ambayo yanapaswa kukamilishwa ndani ya mwaka huu kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani na Uchaguzi Mkuu 2025.
Alisema ACT wataendelea kupigania mabadiliko hayo ili kuwa na uchaguzi ambao hakuna damu ya mtu inayomwagwa.
"Sisi kama viongozi, hatutaki tena kushuhudia vizuka na yatima wakiwa mbele yetu kwa sababu tu kuna watu wachache wanataka mamlaka ya kisiasa," Zitto alisisitiza.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alisema viongozi wa ACT-Wazalendo hawatakubali Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ufanyike kwa kuwa na kura ya mapema, akisisitiza watapambana kuhakikisha utaratibu huo unafutwa.
Pia alisema watapambana kuhakikisha Mkurugenzi wa sasa wa Uchaguzi Zanzibar anaondoka kwenye nafasi hiyo.










