Kuhujumu ujenzi wa vyuo VETA ni kuhujumu  elimu

13Sep 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kuhujumu ujenzi wa vyuo VETA ni kuhujumu  elimu

MOJA ya mikakati ya serikali katika elimu ni kufikisha kila wilaya Chuo cha Elimu ya Ufundi Stadi (VETA), ili vijana kuanzia shule ya msingi hadi wanaohitimu vyuoni wanapomaliza masomo wavitumie na kuwapa ujuzi.

Kutokana na mkakati huo  takribani vyuo 43 vya VETA vimejengwa na vinafanya kazi na pia vipo 39 vinavyokamilishwa ili kwamba awe kijana wa darasa la saba au sekondari, akihitimu aandaliwe ili aweze kujitegemea. 

Mkurugenzi wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Noel Mbonde, anawashauri vijana kuona umuhimu wa kujiunga na vyuo hivyo. 

Taasisi hizo  ni ufunguo zinaweza kuwasaidia vijana kufunguka macho na kuachana na mtindo wa kutegemea kuajiriwa badala yake wajiajiri, hatua mbayo inaweza kupanua ajira zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo wahitimu wamekuwa wakitegemea kupata kazi za maofisini pekee. 

Lakini pamoja na mikakati hiyo ya serikali ya kutaka kuwapa vijana ujuzi kupitia vyuo hivyo, wapo baadhi ya watu ambao huenda wakaikwamisha na kusababisha washindwe kufanikisha kile ilichokusudia. 

Kwa mfano, hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimuagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo kuwakamata wote wanaohusika na usimamizi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA Uyui kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa fedha za mradi huo. Baada ya kuonyesha kutoridhika na gharama za ujenzi wa baadhi ya majengo, kikiwamo kibanda cha mlinzi. 

Ilibainika kuwa ujenzi wa kibanda hicho umegharimu Shilingi milioni 11, na majengo yake kujengwa kwa gharama kubwa tofauti na uhalisia, huku pia akionyesha kutoridhishwa na  nyumba za watumishi chuoni hapo zilizojengwa kwa kiwango kinachotia mashaka. 

Nyumba moja ina uwezo wa kuchukua familia mbili, inajengwa kwa gharama ya Shilingi milioni 114 na tayari wameshatumia zaidi ya Sh. milioni 70, lakini bado ujenzi huo haijakamilika taarifa zinaeleza. 

Kutokana na kutoridhishwa na ujenzi wa chuo hicho unaosimamiwa na VETA, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dk. Batilda Burian, ausimamie ili kazi ikamilike kwa wakati. 

Wakati umefika waliopewa dhamana kwenye miradi ya maendeleo ya umma watambue kushindwa kuisimamia ni sawa na kukwamisha maendeleo ya wanafunzi na nchi kwa ujumla kuwafedhehesha Watanzania. 

Serikali inajenga vyuo hivyo, ili vijana waone  umuhimu wa kujiunga, wasihangaike mitaani, kutokana na kwamba wakifika VETA, wanajifunza ujuzi wa aina yoyote wanaoupenda. 

Zinapojitokeza tuhuma za aina hiyo katika ujenzi wa vyuo, ni wazi zinaweza kukwamisha mikakati ambayo serikali imejiwekea kwa ajili ya kupunguza wimbi la vijana mitaani, wasio na ajira. 

Kwa mfano, Dk. Mbonde anasema serikali imetoa Sh. bilioni 100 kwa lengo la kutaka vijengwe vyuo vingine 36 vya wilaya, ili kufikia zaidi ya vyuo 100 ifikapo mwisho wa mwaka ya kesho. 

Ninaamini kuwa VETA inakuza ujuzi na ubunifu wa vijana kwa ajili ya kuwasaidia kujiajiri na hata wengine kuajiriwa kwa urahisi kutokana na ubunifu wao, hivyo ninadhani si vizuri juhudi hizo za serikali kuhujumiwa. 

Kimsingi, VETA inafungua fursa za ujuzi na ajira kwa vijana, hivyo ingependeza kama wale wanaotamani kujinufaisha kwa fedha zaa ujenzi wa vyuo hivyo wataachana na tamaa hiyo na kusimamia ujenzi inavyotakiwa. 

Mahitaji ya kupata ujuzi kwa Watanzania, hasa vijana kuwa makubwa huku yakizidi kuongezeka kila uchao, ninadhani ndio sababu ya kuifanya kuja na mkakati wa kuwa na chuo kila wilaya. 

Hivyo, ingekuwa vyema iwapo wale wanaotamani kufanya hujuma wakajiweka pembeni, ili lengo la serikali la kutaka kuwapa ujuzi vijana wa Kitanzania na kuwawezesha kujiajiri liweze kutimia.