NBA Afrika, Moet Hennessy wakabidhi uwanja kikapu, Ilala

11Sep 2022
Faustine Feliciane
Nipashe Jumapili
NBA Afrika, Moet Hennessy wakabidhi uwanja kikapu, Ilala

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija amesema kukamilika kwa ukarabati wa uwanja wa mpira wa kikapu wa Spider katika manispaa yake kutatoa fursa ya vijana wengi kucheza mchezo huo na kuongeza hamasa ya michezo kwenye wilaya hiyo.

Ludigija ameyazungumza hayo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa uwanja huo uliofanyiwa ukarabati mkubwa na Kampuni ya Moet Hennessy kwa ushirikiano na NBA Afrika.

Ludigija alisema Wilaya ya Ilala ni kitovu cha michezo katika Mkoa wa Dar es Salaam hivyo uwepo wa uwanja huo uliokaratabiwa kwa kiasi kikubwa  umezidi kuiongezea sifa Ilala.

"Tunafahamu wote kuwa michezo kwa sasa ni ajira kuwepo kwa viwanja vingi vya michezo mbalimbali kunatoa fursa kwa vijana wengi kujikita kwenye michezo, lakini pia haya yanayofanywa pia ni kuunga mkono juhudi za Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan ambaye ameweka wazi mapenzi yake kwenye michezo ," alisema Lubigija.

Alisema taarifa aliyonayo kiwanja hicho ni cha nne kujengwa Afrika na cha kwanza ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa  Kampuni ya Moet Hennesy iliyoshirikiana na NBA Afrika kukarabati uwanja huo,  Janet Mwalilino, alisema kuwa mchakato wa ukarabati wa uwanja huo ulianza muda mrefu baada ya kukutana na NBA Afrika na wanafurahi kuukabidhi baada ya ukarabati mkubwa walioufanya.

"Huu ni uwanja wa kwanza Afrika Mashariki, tumefanya hivi kwa kushirikiana NBA Afrika katika nchi za Nigeria, Ghana na Cameroon lakini kwa Afrika Mashariki, huu ndio uwanja wa kwanza," alisema Janet.

Aidha, alisema baadhi ya vitu walivyoviongeza kwenye Uwanja huo ni taa ili kuwawezesha watu kucheza mpira wa kikapu kwa muda wanaoutaka wao hata usiku.

Mbali na taa za uwanja, pia wamejenga majukwaa kuwawezesha mashabiki kukaa na kufuatilia mchezo huo pamoja na eneo la kucheza.

Uwanja huo kwa muda mrefu umekuwa ukitumiwa na klabu za Spider na Old Guard ambazo pia zitaendelea kuutumia baada ya ukarabati huo.

Mwenyekiti wa Klabu ya Spider, Lwaga Nikipula, alisema kwa sasa wanajipanga kutafuta mbinu ya kujenga majengo ya kubadilishia nguo.

"Tunashukuru sana kwa ukarabati huu, kwa sasa  tunaangalia namna ya kutafuta wafadhili, wanaweza wakawa hawa hawa wenzetu wa Hennesy na NBA Afrika au kampuni nyingine watusaidie kujenga majengo ya kubadilishia nguo kwa wachezaji, mchakato huo tumeuanza kwa kuomba kibali serikakini kwa sababu maeneo haya yapo chini yao tumeshaandika barua huko alisema Lwaga.

Alisema licha ya kuendelea kuutumia uwanja huo, lakini upo chini ya serikali.