Akizungumza mara baada ya kuzindua ofisi hizo Meneja wa Mamlaka ya Mapato mkoani humo Jacob Mtemang'ombe, amesema eneo hilo lina wafanyabiashara wengi na linakua kiuchumi ndiyo maana imeamua kuwasogezea huduma hiyo.
"Mpaka sasa tuna wafanyabiashara 550 ambao tumewasajili kwenye mfumo lakini wako wengi zaidi ya hao kwa sababu kama nilipoeleza hapo mwanzo eneo hili halikua covered vizuri kwasababu ya umbali kwa ofisi hii kuwa karibu tunaamini tutawafikia walipa kodi walio wengi,"alisema Mtemang'ombe.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Mlele Lincolin Tamba aliyekuwa mgeni rasimi katika ufunguzi huo akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo amewataka wafanyabiashara hao kutumia fursa hiyo itakayo wasaidia kupata huduma ya kodi kiurahisi.

Nae Mwakilishi wa Jumuiya ya wafanyabiashara mkoani Katavi Jonas Amos, amesema walikua wakitembea kilometa 100 hadi 300 kila siku kufuata huduma hiyo.
"Ilitulazimu kulala huko tulitumia gharama kubwa, ila kwa sasa tumeokoa muda na fedha zetu hatutahangaika tena tutalipa kodi kwa wakati," amesema Amos.
Grace udoba ni mfanyabiashara wa Majimoto amesema ukosefu wa ofisi ya kulipa kodi iliwaathiri kwa kiasi kikubwa na kusababisha kuingia mgogoro na serikali kwakuonekana hawalipi kodi.










