Kati ya vyuo hivyo vingine vilibainika kuwa havina walimu wenye sifa, mazingira mabaya ya kujiendeshea, ukosefu wa nyenzo huku vingine vikibainika kwamba mchana vimekuwa vikiendesha shughuli za chuo kama kawaida na usiku kubadilika kuwa baa na sehemu ya maonyesho ya mechi ya mpira.
Kadhalika, Necta limevipa wiki mbili vyuo 41 kujisajili mara moja kwenye baraza hilo kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria baada ya kubainika kujiendesha bila usajili huo.
Vyuo vingine ambavyo vimepewa onyo na kutakiwa kujirekebisha mara moja ni 11 ambavyo vimesajiliwa, lakini vinaendesha programu za kutoa kozi nyingine zaidi ya zile zilizosajiliwa.
Katika orodha hiyo, vyuo 112 vimebainika vilikuwa vinajiendesha wakati usajili wake umekwisha muda wake, huku vyuo 52 ithibati yao ilibainika kuwa imeisha, na vyote vimepewa muda wa mwezi mmoja kuhakikisha vinarekebisha kasoro hizo kabla hatua nyingine hazijachukuliwa.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Steven Mlote, alisema vipo vyuo vingi ambavyo vilibainika kujiendesha katika mazingira mabovu na kukitaja chuo cha State College of Health and Alliance Sciences cha Dar es Salaam, kuwa ni miongoni mwa vyuo vinavyojifanya mchana vyuo na usiku kuendesha shughuli za baa na kwamba vingine vilibainika kukutwa na mabango ya kuonyesha mechi za mpira.
Tunaipongeza Nacte kwa ukaguzi uliobaini madudu hayo ambayo ni aibu na umebainisha kuwa bado watu kadhaa wanaichukulia elimu kama suala la mchezo.
Hata hivyo, inaonekana dhahiri kwamba ukaguzi wa kina na endelevu haujafanyika kwa kuwa kama ungekuwa unafanyika kila wakati, hali isingefikia hapa.
Sisi kama taifa tumedhamiria kwa dhati kufufua kiwango cha elimu nchini kilichoporomoka kwa kasi, tunapaswa kuwa makini kwa kuweka taratibu, sheria na kanuni ngumu ili ziwabane wale wote watakaoomba usajili wa kumiliki shule na vyuo.
Hatua hiyo itasaidia kuwasajili wale ambao ni makini na wenye dhamira ya dhati ya kutoa elimu badala ya kusajili wababaishaji ambo lengo lao ni kuwatapeli fedha na kuwapotezea muda wazazi na walezi wa vijana wanaoandikishwa.
Tunaishauri Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi pamoja na Nacte kufanyia kazi matokeo ya ukaguzi huo kisha kuja na ufumbuzi ambao sisi Nipashe tunaona kuwa ni kubadili sheria, kanuni na taratibu za usajili wa shule na vyuo.
Tunapendekeza kwamba muda wa ukaguzi wa shule na vyuo uongezwe; kwa maana kwamba uwe ukifanyika kila wakati na wamiliki ambao shule na vyuo watabainika kukiuka masharti ya usajili wanachukuliwa hatua kali hususani kufutiwa leseni ili liwe fundisho kwa wengine.
Kugeuza chuo mchana kuwa sehemu ya kusomea na jioni kuwa sehemu ya burudani ni kuwasababishia adha na usumbufu wanafunzi, walimu na wafanyakazi.
Kadhalika, litakuwa jambo bora kama wamiliki watawekewa masharti kwamba walimu wanaofundisha katika vyuo hivyo wawe ni wale ambao wamethibitishwa na bodi husika za wataalamu.
Kama ni mhandisi awe amethibitishwa na bodi ya wahandisi, hivyo hivyo na taaluma nyingine kinyume cha hapo asiruhusiwe kufundisha katika vyuo hivyo.
Tunaipongeza Nacte kwa hatua ilizozichukua na tunaishauri isilegeze kamba, kwa kufanya hivyo, wahusika wataendelea kuutumia udhaifu huo kwa manufaa yao.










