Kwenye mechi hiyo ya watani wa jadi iliyokuwa maalum kwa ufunguzi wa Ligi Kuu msimu wa 2022/23, Simba ilitawala zaidi kipindi cha kwanza na Yanga kuwakimbiza wapinzani wao kipindi cha pili, lakini hadi mwisho mshindi wa ngao msimu uliopita akatoka uwanjani na mabao 2-1.
Ilioneka kabisa kuwa bado Simba ina tatizo kubwa kwenye eneo lake la viungo wakabaji, kwani wachezaji wa Yanga wakiamua kuondoka, basi wanawafikia kwa urahisi mabeki wa Simba, au kipa wao Beno Kakolanya.
Ni eneo ambalo linaonekana sugu na halijapatiwa majibu kwenye kikosi cha Simba, kwani pamoja na kuonekana dhahiri msimu uliopita, hata kwenye mechi ya Simba Day dhidi ya St George lilionekana pia.
Na kama si uhodari wa kipa Kakolanya aliyeokoa mabao yapatayo matatu ya wazi kutoka kwa mastraika wa Yanga, Stephane Aziz Ki na Mayele, basi Simba ingeoga mabao mengi.
Pia beki Mohamed Outtara alifanya kazi kubwa kwenye mechi ya jana, akishirikiana na Henock Inonga, lakini hawakuwa na watu wa mbele wazuri wa kuwalinda.
Simba ilianza kupata bao dakika ya 15 kupitia kwa mchezaji wa kimataifa wa Senegal, Pape Sakho alipoiandikia Simba bao la kuongoza, baada ya pasi ndefu ya Chama kutoka winga ya kushoto kukatiza mpaka winga ya kulia, huku mabeki wa Yanga wakiwa wamesimama kutengeneza mtego wa kuotea, kiungo huyo alitoka nyuma na kuunganisha mpira bila kutuliza, ukimpita kipa Diarra na kukwama wavuni.
Aziz Ki, nusura aisawazishie Yanga dakika ya 23, kama si uhodari wa kipa Kakolanya kuruka na kuliwahi shuti lililopigwa na kiungo huyo ambalo lilikuwa likielekea wavuni.
Hiyo ilitokana na nona fupi iliyopigwa na wachezaji wa timu hiyo na kumpa kiungo huyo aliyesajiliwa msimu huu akitokea Asec Mimosas.
Diarra aliiokoa Yanga kufungwa bao la pili dakika ya 38, alipodaka kwa ustadi mpira wa kichwa uliopigwa na Sadio Kanoute, kutokana na mpira wa faulo uliopigwa na Sakho.
Mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili kwa timu zote kwa kiasi kikubwa yaliisaidia Yanga, kwani iliamua kupita kati baada ya kocha Nasreddine Nabi kugundua udhaifu kwenye nafasi ya kiungo mkabaji wa Simba, akimhamisha Aziz Ki kutoka pembeni na kumuingiza kati, akawa na kazi ya kuchukua mipira na kuanza kutembea kati akiwa hakabwi na wakati anafikiwa na mabeki wa Simba, anagawa mpira kwa Mayele au Bernard Morrison ambao walikuwa wanatengeneza hatari kubwa kwenye lango ya wapinzani.

Kwenye mechi ya jana, Yanga ndiyo ilianza kulifikia lango la Simba dakika ya saba ya mchezo kwa krosi iliyopigwa na Farid Mussa na kuleta kizaazaa kwenye lango, kabla ya kufagiliwa na Mohamed Outtara.
Simba ilijibu dakika moja baadaye, baada ya Clatous Chama kuondoka na mpira kutoka katikati ya uwanja, na kummegea pande Kibu Denis ambaye alipiga shuti, lakini kipa Djigui Diarra alikuwa makini akaudaka mpira huo.
Kibu kwa mara nyingine tena alikosa bao la wazi dakika ya 11, alipounganisha krosi ya Israel Mwenda kutoka winga ya kulia, akiwa anatazamana na kipa Diarra, alipiga nje huku akiwa amezongwa na mabeki wa Yanga.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Yanga kutwaa Ngao ya Jamii, lakini ikiwa ni mara ya nne kwenye mechi sita ilizocheza dhidi ya Simba.
Mara ya kwanza ilikuwa ni 2001, Yanga ikishinda mabao 2-1, na 2010 Yanga ilitwaa tena kwa kuifunga kwa mikwaju 3-1 ya penalti, baada ya dakika 90 za suluhu, mwaka jana ikiwa ni mara taatu, kabla ya kuchukua tena mwaka huu.
Simba imefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii mara mbili tu mbele ya Yanga, 2011 ikishinda mabao 2-0 na mara ya pili ilikuwa mwaka 2017 kwa mikwaju 5-4 ya penalti.
SIMBA YAWAHI KUINGIA
Wakati kikosi cha Simba kiliwasili uwanjani saa 11:09 jioni, watani zao Yanga walitia timu dakika 12 baadaye kupitia mlango wa dharula.
Kama ambavyo imekuwa ada pindi timu hizo ziwasilipo kwenye dabi, ndivyo ilivyokuwa muda mfupi kabla ya kikosi hicho cha Wananchi kuwasili.
Makomandoo walijipanga kandokando ya sehemu ambayo gari la timu kubwa lilipotakiwa kupaki kiasi cha kuzua taharuki.
Baadhi ya mashabiki ambao walikuwa wakikatisha eneo hilo, iliwabidi kusogea ili kuona mastaa wao lakini ilikuwa tofauti kwani alionekana kushuka kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi na viongozi wengine.
Wachezaji hawakuonekana kushuka na tulipofanya utafiti tukabaini kuwa hakuna mchezaji ambaye alikuwepo ndani.
Basi la nyuma ya lile ambalo wengi waliamini lilikuwa na wachezaji ndilo ambalo lilielezwa kuwa lilikuwa na nyota wa kikosi hicho.
Muda mchache baadaye ndipo shangwe lilipoibuka ndani kwani nyota wa Yanga wakiongozwa na Fiston Mayele walikuwa wakiingia kwa mlango usio rasmi (dharula) ambako limekuwa likipaki gari la zimamoto.
Mashabiki wa Yanga walishangilia hadi wachezaji wao walipoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Imeandikwa na Saada Akida na Adam Fungamwango.










