Serikali sasa iiwezeshe Bodi ya Utalii kwa bajeti

04Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali sasa iiwezeshe Bodi ya Utalii kwa bajeti

KUNA taarifa kuwa Bodi ya Utalii nchini (TTB) inakabiliwa na uhaba wa fedha kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii.
Hali hiyo ilielezwa na Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo, kwamba amekuta fedha kidogo katika akaunti zake.

Jaji Mihayo alisema akaunti za TTB zina Sh. milioni 11 na Dola za Marekani 6,000 (Sh. milioni 13.12). Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema bodi hiyo ina deni la Sh. bilioni 3.7 zilizotumika kutangaza utalii ndani na nje ya nchi.

Waziri Maghembe pia alisema wafanyakazi wa bodi hiyo wanadai Sh. milioni 396 ambazo ni malimbikizo mbalimbali ya stahili zao.

Jaji Mihayo alisema wameingia na kukuta bodi ikiwa kwenye hali mbaya kifedha pamoja na deni hilo ambalo wanatakiwa kulilipa.

Alisema katika deni hilo, Sh. bilioni 2.5 ni madeni ya nje ya nchi ambayo wametangaza utalii; ikiwamo nchini Uingereza.

Deni la ndani ni Sh. bilioni 1.2 na kwamba wadai wa ndani walilifikisha mahakamani na hukumu iliyotolewa iliwataka TTB kulilipa deni hilo.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Mihayo alisema wapo watumishi watatu walioacha kazi kutokana na ugumu.

Hali mbaya ya fedha ya bodi hiyo inatishia uhai wake na kuzua shaka kama itaweza kutekeleza jukumu lake la msingi la kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje.

Kazi ya kutangaza vivutio vya utalii nje na ndani ya nchi inahitaji fedha za kutosha na kinyume chake haiwezekani na matokeo yake ni nchi kukosa fedha nyingi za watalii wanaokuja nchini.

Itakumbukwa pia kwamba utalii ni moja ya sekta zinazoingizia taifa fedha nyingi za kigeni na kuchangia katika uchumi.

Baadhi ya nchi jirani na Tanzania zimekuwa zikiwekeza fedha nyingi katika kutangaza vivutio vyao vichache vya utalii nje na ndani, na matokeo yake zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuongeza idadi ya watalii sambamba na kupata pato kubwa kutoka sekta ya utalii. Jitihada zao zimesababisha baadhi ya vivutio vya nchi zingine ikiwamo Tanzania kujulikana kuwa viko katika nchi hizo.

Kinachotakiwa kufanywa na Serikali ni kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya TTB, bodi hiyo kuwa na mikakati, mipango mizuri na endelevu pamoja na kuwa wabunifu katika kutangaza vivutio vyetu vya utalii.

Tunaishauri pia TTB ibadilike katika utendaji wake kwa kuwa wawazi na waadilifu kwa sababu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15 ilionyesha utata katika malipo ya bodi hiyo kwenda katika klabu za soka za Sunderland ya Uingereza na Seattle Sounders ya Marekani.

Kadhalika, TTB ijiepushe kuingia katika mikataba mibovu ambayo matokeo yake ni kuingia katika hasara na madeni yasiyolipika.

Kwa kuwa Waziri Maghembe ameahidi kuwa Serikali itazishughulikia changamoto zinazoikabili TTB ikiwamo kulipwa kwa deni, ni matarajio yetu kuwa bodi hiyo itajipanga upya na kutangaza vivutio vya utalii nje na ndani kwa kasi kubwa.

Hilo likifanyika, bila shaka itatimiza agizo la Serikali la kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni moja hadi tatu kwa miaka miwili ijayo.

Suala la kutangaza utalii limo katika sera yetu ya sasa ya nje ya diplomasia ya uchumi, ambayo inahimiza kutangaza fursa za kiuchumi zilizoko nchini.